Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan imepanga kuikabidhi Magari mawili ya kubebea wagonjwa Wilaya ya Karatu.
Hayo yamesema na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango wakati akiweka jiwe la msingi katika hospitali ya Wilaya ya Karatu.
"Serikali imeweka nguvu kubwa katika kuhakikisha miundombinu ya sekta ya afya inaimarika zaidi na kuwezesha utoaji wa huduma bora".
Aidha, Dkt.Mpango amesema ndani ya miezi miwili Serikali italeta watumishi wasiopungua 25 katika sekta afya ili kuzifanya hospitali hizo kuendelea kutoa huduma bora na kwa wakati.
Amewataka wananchi wa Karatu kuhakikisha wanaitunza hospitali hiyo iliyogharimu fedha nyingi na walinde vifaa vya hospitali hiyo.
Pia, Serikali inaendelea kuhakikisha hospitali za Wilaya zinatoa huduma bora ikiwemo upatikanaji wa Dawa na vifaa tiba na viongozi wa wilaya wavisimamie.
Amewataka wale wote watakaobainika wameiba vifaa wakamatwe na wafikishwe katika vyombo vya sheria kwani watakuwa wamehujumu uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema nguvu kubwa imewekwa na Serikali katika sekta ya afya na kiasi cha Trilioni 1.3 zilitolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya katika miundombinu na vifaa tiba.
Naye Naibu Katibu Mkuu Tamisemi,anayeshughulikia suala la Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe, Dkt.Charles Mahera alitoa rai kwa wananchi kulinda vifaa vya hospitali kwani baadhi za hospitali za wilaya vifaa huibiwa.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Rajabu Karia alisema hospitali hiyo imeanza kutoa huduma baada ya kukamilika kwa majengo tisa ikiwemo jengo la wagonjwa wa nje na jengo la maabara lakini pia wanatarajia kutoa huduma za uzazi ili wananchi waanze kujifungua katika hospitali hiyo
Alisema ingawa hospitali hiyo imeanza kutoa huduma lakini bado kunachangamo zinazoendelea ya upungufu wa watumishi pamoja na samani na vifaa tiba kweye majengo yaliyokamilika na kuongeza kuwa hospitali hiyo imegharimu sh.bilioni 3.379.
Uzinduzi wa hospitali ya wilaya ni miongoni mwa shughuli zilizofanywa katika ziara ya kikazi ya Makamu wa Rais Dkt. Mpango katika Wilaya ya Karatu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.