Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa Paul Christian Makonda amewahidi wakazi wa Mko wa Arusha, kusimamia haki ya kila mwananchi na yupo tayari kupoteza chochote alichonacho ilimradi, mwananchi mmoja, aweze kupata haki yake na kunufaika na cheo chake.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Makonda akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye Kliniki ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi amesema hawezi kukaa kwenye kiti cha Mkuu wa Mkoa ilihali wananchi anaowaongoza wakiteseka na changamoto mbalimbali ambazo zipo ndani ya Mamlaka yake ya Kiuongozi.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi hao pia kung'ang'ana kudai haki yao, Akisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wanasheria bingwa kutoka Ofisi zaidi ya 75 za Mawakili ili kuwasikiliza na kuwapa misaada ya kisheria.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Makonda ametumia fursa hiyo pia kusema kamwe katika uongozi wake Mkoani Arusha hatokubali kuendelea kuona vilio vya Wana Arusha waliokata tamaa kutokana na kutosikilizwa kero zao na kutatuliwa akiahidi kuijenga Heshima yake kwa kurejesha haki kwa Wana Arusha walionyang'anywa haki zao.
Mhe. Mkuu wa mkoa ametumia fursa hiyo pia kusema anatamani Mkoa wa Arusha uwe Mkoa wenye hofu ya Mungu, wenye kuthamini mtu kwa utu wake pamoja na kutamalaki kwa Haki kwa kila mkazi wa Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa