Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amewataka wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya za Arusha kuhakikisha miradi yote itakayotekelezwa chini ya mradi wa BOOST iwe bora na ikamilike kwa wakati.
Ameyasema hayo alipokuwa akiwasainisha mikataba ya utekelezaji wa mradi wa BOOST wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi.
Amesema Mkoa umepokea jumla ya Bilioni 6.815 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa shule za awali na msingi (BOOST) Arusha.
Pia, amewahasa wakafanye kazi kwa mshikamano na waunde timu zitakazokuwa na nidhamu katika utekelezaji wa mradi huo.
Katibu Tawala Mkoa Missaile Musa amesema mradi huo wa BOOST utaenda kujenga shule mpya za msingi 7, vyumba vya Madarasa 109, vyumba vya madarasa ya mfano ya elimu ya awali 14.
Vilevile, Vyumba vya Madarasa ya elimu Maalum 2, Matundu ya Vyoo 90, Nyumba za Walimu 3( two in one) na ukarabati wa Shule Kongwe 1.
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa Wilaya wote, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Raymond Mangwala amesema wataenda kuisimamia mikataba hiyo kwa umakini na kufuata taratibu zote ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezeka ndani ya muda.
Mradi wa BOOST umeanza kutekelezwa Aprili 1 na unatarajiwa kukamilika Juni 30,2023 katika halmashauri zote za Mkoa wa Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.