Na Elinipa Lupembe.
Vijiji 351 vya mkoa wa Arusha, sawa na asilimia 95.38 vimefikiwa na miundombinu ya umeme, huku wakandarasi wakiendelea na kazi ya kukamilisha usambazaji wa umeme kwenye vijiji 17 vilivyosalia ili kukamilisha vijiji vyote 368 vya mkoa huo na kufikia asilimia 100.
Hayo yamethibitishwa na mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella, alipopata fursa ya kuzungumza, muda mfupi kabla ya kumkaribisha, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko, alipotembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusafirisha Umeme cha Lemuguru - mkoani Arusha.
Mhe. Mongella, kwa niaba ya wananchi wa mkoa huo, ameishukuru Wizara ya Nishati na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuijali Arusha, kwa kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo huku ikitoa kipaumbele kwa kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ya umeme kupitia mradi wa umeme vijijini (REA), miradi ambayo iko hatua za ukamilishaji na kuvifikia vijiji vyote 368 vya mkoa wa Arusha.
"Kwa sasa Mkoa wa Arusha unakamilisha ufungaji wa umeme kwenye vijiji 17 vilivyosalia, huku wakandarasi wakijikita katika kuendelea kusambaza umeme kwenye vitongoji na kuwafikia watumiaji, jambo ambalo linachochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla wake" Ameweka wazi RC Mongella
Ameongeza kuwa matokeo ya uwepo wa umeme Arusha, yameanza kuonekana wazi, kupitia mabadiliko katika pato la wananchi sio kwa kuwaka tuu, bali kukuza uchumi wa mkoa, huku uanziashwaji wa viwanda vidogo ukiendelea, na wananchi kulazimika kujikita katika shughuli za uzalishaji, shughuli zinazosababisha, uwepo wa amani na utulivu katika mkoa huo.
"Nikiri wazi kuwa, wananchi wa Arusha wamenufaika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025, ikitekelezwa kwa asilimia 100 na kufikia lengo la serikali la kuhakikisha huduma za Umeme, zinawafikia wananchi kwenye maeneo yao hususani wananchi waishio vijijini" Amethibitisha Mhe. Mongella.
Awali mradi wa Kituo cha Umeme Lemuguru, unatekelzwa na serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 14.295, ukiwa umefika asilimia 30 na unategemea kuhusambaza na kuongeza upatikanaji wa huduma za umeme kwa wananchi wa maeneo ya Longido, Monduli, Arumeru pamoja na Jiji la Arusha.
#ArushaFursaLukuki
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.