Kamati ya ushauri ya Mkoa wa Arusha imepitisha bajeti ya shilingi Bilioni 388.6 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali za Mkoa na Halmashauri zake 7.
Bajeti hiyo umepitishwa katika kikao cha ushauri cha Mkoa, kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkoa.
Katika bajeti hiyo jumla ya shilingi Bilioni 259.5 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi Bilioni 129.1 ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika Mkoa.
Akisoma bajeti hiyo kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa, Katibu Tawala msaidi Mipango na uratibu bwana Said Mabiye amesema bajeti hiyo imezingatia utekelezaji wa mambo mbalimbali ikiwemo; mishahara ya watumishi, utoaji wa mikopo ya 10%, miradi mbalimbali ya maendeleo ya ujenzi na uboreshaji wa vituo vya afya, ujenzi wa vyumba vya madarasa Barabara na huduma za Maji.
Katika kuhakikisha bajeti hiyo inatekelezeka na Mkoa wa Arusha unafanikiwa kwa kiwango kikubwa, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongella amesisitiza mambo haya; amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha wanachukua hatua kali kwa wale wote watakaohusika na upotevu wa madawa.
Pia, amewataka wakuu wa wilaya wasiruhusu uwazishwaji wa maduka ya madawa binafsi karibu na vituo vya afya na hospitali zote ili kupunguza upotevu wa madawa katika hospitali hizo.
Mongella amesisitiza zaidi kwa yeyote atakaye bainika anatoa hati ya ardhi katika Barabara za akiba na maeneo mengine yasiyostahili wachukuliwe hatua kali.
Kikao cha ushauri cha Mkoa kilikuwa maalumu kwa ajili ya kupitisha bajeti ya Mkoa kwa mwaka 2022/2023 na kushauri mambo mbalimbali ya maendeleo kwa Mkoa wa Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.