Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Balozi Emmanuel John Nchimbi, amesema Edward Ngoyai Lowassa alikuwa ni mtu aliyependa kufanyakazi, alikuwa ni mchapakazi, aliyezitumika nafasi zote alizokuwa nazo kwa weledi mkubwa.
Amesema, licha ya kuwa watu wanaweza kupishana katika maelezo ya kumwelezea
katika mambo mbalimbali, lakini jambo moja ambalo haliwezi kubishaniwa ni jinsi alivyokuwa mchakapakazi wa kweli, katika nafasi zake zote alizowahi kuzitumikia na katika kuwatumikia Watanzania wote.
Dkt. Balozi Nchimbi amesema kupitia uhodari wake wa kuchapa kazi katika kutimiza wajibu wake kwa nchi, Hayati Lowassa alikuwa kiongozi mwenye uthubutu na uwezo wa kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya kutafuta ufanisi na kupata matokeo chanya ya haraka kwa ajili ya maendeleo ya watu.
Dkt. Balozi Nchimbi amesema hayo leo Ijumaa, Februari 16, 2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kufika kuwapatia pole wafiwa, kusaini kitabu cha maombolezo na kutoa heshima za mwisho, nyumbani kwa Hayati Lowassa, katika Kijiji cha Ngarash, wilayani Monduli Mkoa wa Arusha, akiongeza kuwa kutokana na sifa za kiuongozi alizokuwa nazo, kifo cha kiongozi huyo ni pigo kubwa kwa nchi.
“Lowassa alikuwa mchapakazi kweli kweli. Alikuwa mtu wa maamuzi magumu. Watu wanaweza wakapishana katika kila maelezo wanayotoa kuhusu Lowassa lakini hakuna hata mtu mmoja anayeweza kuwa na ujasiri wa kusema alikuwa mvivu, au alikuwa hapendi kufanya kazi au hakuwa na mapenzi na nchi yake, hakuna. Alikuwa mchapakazi wa hali ya juu. Hakupoteza muda hata mara moja kuacha kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania.
“Alikuwa mzalendo, mnyenyekevu na aliyependa watu wote bila kuwabagua. Moja ya uamuzi mgumu unaoendelea kukumbukwa ni hatua ya kiongozi huyo aliyoichukua ya kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008,” amesema Dkt. Nchimbi.
Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Nchimbi amesema taarifa za msiba huo wa Waziri Mkuu Mstaafu Lowassa, ilikuwa ni mojawapo ya habari mbaya kwake kuwahi kuzipata.
“Nimepoteza rafiki, kaka na mlezi. Lakini pia nimeona jinsi ambavyo chama changu kimepoteza mtu. Nimeona pia jinsi ambavyo nchi yetu imepoteza mtu. Nimeona jinsi ambavyo vyama vingine vilivyokuwa karibu naye vimepoteza mtu muhimu kwao. Pigo hili nililihisi binafsi na niliona ambavyo linaathiri nchi yetu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.