Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Missaile Musa amesema kupanuliwa kwa barabara ya Arusha-Kisongo kutasaidia kuongeza usalama katika barabara hiyo.
Bwana Missaile amezungumza hayo alipokuwa akifunga kikao cha usanifu wa barabara hiyo kilichofanyika Jijini Arusha.
Amesema, barabara hiyo ni muhimu kwa Mkoa wa Arusha kwasababu ni Mkoa wa Kitalii hivyo ujenzi hui utasaidia kupendezesha muonekano wa mji hususani kwa watalii wanashuka katika kiwanja cha ndege cha Kisongo kuelekea mjini.
Umuhimu mkubwa wa barabara hiyo nikurahisisha ufikaji wa watu katika uwanja wa Ndege wa Kisongo.
Kwa Upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha Mhandisi Reginald Massawe amesema wanaenda kujenga barabara itakayoanzia Soko la Kilombero kwenda uwanja wa ndege wa Kisongo kwa njia nne na kipande cha barabara inayoanzia chuo cha ufundi Arusha hadi kona ya Ngarenaro.
Lengo la kujenga barabara hiyo nikupunguza msongamano wa Magari katika barabara hiyo, pia kuhamisha barabara hiyo katika eneo la uwanja wa Kisongo ili kupisha uwanja huo uweze kufanyiwa maboresho zaidi na kuruhusu Ndege ziweze kutua hadi usiku.
Kwasasa katika uwanja huo watalii wanaruhusiwa kutua mwisho saa 12 jioni lakini baada ya maboresho hayo ndege zitaweza kutua hadi usiku.
Katika kikao hicho wameweza kuwashirikisha meneja wengine kutoka katika baadhi ya taasisi za Serikali kwa lengo la kutoka na mpango wa pamoja.
Amesema mradi huo kwa sasa upo katika hatua ya upembuzi yakinifu na wanatarajia watamaliza mwanzoni mwa mwezi Agasti na hatua hiyo itagharimu Milioni 250 hadi kukamilika kwake.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Mhandisi Juma Hamsini amewaomba TANROADS Arusha kuzingatia mpango miji wa Jiji la Arusha ili kuweka uwiano kati ya barabara hiyo na mpango wa Jiji la Arusha.
Mradi wa kujenga barabara ya Arusha Kisongo yenye urefu wa km 9.1 ni mpango uliowekwa na Serikali kwa lengo la kuboresha miundombinu ya barabara katika Jiji la Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.