Na Elinipa Lupembe.
Kufuatia mkakati wa Serikali ya awamu ya sita, wa kujenga uwanja wa mpira wa miguu, ikiwa ni maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), yanayotarajiwa kufanyika mapema mwaka 2027, Halmasahuri ya Jiji la Arusha, imetenga Shilingi Bilioni 2.5 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi watakayotoa maeneo yao.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo, kwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Damian Ndumbaro ( MB), Mkurugenzi Mtendaji, Jiji la Arusha, Mhandisi Jumaa Hamsini, amesema kuwa Serikali ilitoa maagizo ya kupatikana Eka 83 na mpaka sasa tayari zimepatikana Eka 39, zikiwa zimeandaliwa Hati Miliki, huku Jiji la hilo likitenga shilingi Bilioni 2.5, kwa ajili ya kulipa fidia wananchi watakaopisha maeneo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo wa mpira.
Amesema kuwa, tayari hatua zote zimeshafanyika, na Jiji limetenga kiasi hicho cha fedha, ambacho kitatumika kulipa fidia kwa wananchi ili kupata eneo la Eka 44 zitakazokwenda kukamilisha Eka 83 zinazotakiwa na Serikali ili kutekeleza ujenzi huo.
"Sisi kama Jiji la Arusha, tumeshajipanga vema, kuhakikisha adhma ya Serikali ya awamu ya sita, inafikiwa kwa kiwa na uwanja wa mashindano, viwanja vya mazoezi pamoja na miundombinu yote inayohitajika inajengwa hapa Mtaa wa Murongoine kata ya Olmoth na tutahakikisha mashindano hayo yatafanyika kama yalivyopangwa".Ameweka wazi Mhandisi Hamsini.
Awali, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, ametembelea na kukagua eneo linaloandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa mpira na viwanja vya mazoezi, na hatimaye Jiji la Arusha kumkabidhi mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella Hati Miliki ya Eka 39 na Kumkabidhi Waziri huyo mwenye dhamana.
Ikumbukwe kuwa ujenzi wa uwanja wa mpira wa kimataifa mkoani Arusha, licha ya kuwa ni kwa ajili ya mashindano ya kimataifa ya AFCON lakini zaidi ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi unaokwenda kuwekeza kwenye utalii wa michezo katika mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla wake.
#arushafursalukuki
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.