Akiwa Kisongo Mjini Arusha Kwenye Mkutano wa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda alipata fursa ya kujibu baadhi ya maswali yaliyoelekezwa kwake na Dkt. Nchimbi.
Mkuu wa Mkoa amekiri kwamba barabara nyingi za Jiji la Arusha ni mbovu,na nyingine huharibika zaidi nyakati za Mvua lakini akaahidi kwamba tayari wamepata mpango wa kujenga takribani Km.100 za Lami pamoja na Km.2000 za changarawe na barabara za vumbi na tayari wameanza upembuzi wa kubaini barabara gani za kuanzia kwenye awamu hii ya kwanza.
Kadhalika ameagiza wenyeviti na watendaji wa serikali kuwa walinzi namba moja wa maeneo yao kwa kutoa taarifa kuhusu wahalifu na uhalifu katika maeneo yao kutokana na uwepo wa matukio ya wizi na udokozi kwenye baadhi ya maeneo ya mkoa wa Arusha akilitaka Jeshi la polisi pia kuimarisha doria kwenye maeneo yenye matukio hayo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa ameahidi kwenda Kisongo siku ya Jumanne ya wiki hii ili kwenda kuwasikiliza na kutatua kero za wananchi wa eneo hilo. Hatua hii imekuja mara baada ya wananchi hao kumuomba Mkuu wa Mkoa kufika kwenye eneo lao.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.