Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Waheshimiwa Madiwani nchini kuiga mfano wa Diwani wa Kata ya Kiutu Mhe. Malaki Malambo aliyetoa kiwanja chenye ukubwa wa zaidi ya mita za mraba 6,400 kwa ajili ya kujenga shule ya Sekondari Kiutu Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.
Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo kwa madiwani wote nchini, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua na kuhimiza utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri za Mkoa wa Arusha.
Amesisistiza kuwa, kitendo cha Diwani wa Kata ya Kiutu Mhe. Malambo kutoa kiwanja chake ni ishara ya upendo wa dhati alionao kwa wananchi ambao walimchagua ili awaongoze na kuwaletea maendeleo.
“Ninawaomba Madiwani nchini wengine kuiga mfano mzuri wa Mhe. Malambo aliyejitoa kwa wananchi wake kwa kutoa kiwanja kilichowezesha ujenzi wa shule ya Sekondari Kiutu, hii ndio uhalisia wa kuwatu’ikia wananchi". Amesisitiza.
Ili kuunga mkono jitihada wa Mhe. Malambo na wakazi wa mkoa wa Arusha, Waziri Mchengerwa ameanisha kuwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI itafanya mchakato wa kuwezesha kukamilisha ujenzi wa jengo la Shule ya Kiutu ili shule hiyo mwakani ipokea wanafunzi zaidi ya 500 tofauti na mwaka huu ambapo imepokea wanafunzi 400.
Mhe. Mchengerwa amesema majengo 8 yaliyokamilika hayawezi kuchukua wanafunzi zaidi ya 400, hivyo kuna uhitaji mkubwa wa kukamilisha majengo yaliyosalia ili wanafunzi wapate miundombinu bora na rafiki ya kuwawezesha kutimiza ndoto zao.
“Nikihitimisha ziara yangu, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Ofisi ya Rais-TAMISEMI aje na timu yake kufanya tathmini ya gharama zinazohitajika ili tuwasilishe ombi la fedha kwa Mhe. Rais na hatimaye tuweze kukamilisha ujenzi wa shule hiyo,” Mhe. Mchengerwa amehimiza.
Waziri Mchengerwa yupo mkoani Arusha kwa ajili ya ziara ya kikazi iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo na kuhimiza uwajibikaji kwa wasimasmizi wa miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.