Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, Jinsia, wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewahasa wananchi kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 hasa katika kipindi hiki cha sikukuu.
Ameyasema hayo alipokuwa akizindua mpango harakishi na shirikishi wa utoaji chanjo ya UVIKO 19 awamu ya pili, iliyofanyika Jijini Arusha.
Kuna haja kubwa ya kupambana na huu ugonjwa hasa kwa kujikinga na kuchanja kwani bado kuna ongezeko la wagonjwa kwa sasa.
Takwimu zinaonesha kuwa kati ya wagonjwa 10 wa UVIKO 19 waliolazwa hospitalini saba hawajachanja na watatu wamechanja.
Vifo vinavyitokana na UVIKO 19 kati ya watu 10 saba hufa kwa kutochanja na watatu huwa wakiwa wamechanja.
Kuna umuhimu mkubwa wa kuchanja kwani ugonjwa huo utakuwa mwepesi, na madhara yake ni madogo kulinganisha na asiye chanja.
Amesema kampeni hiyo ya 2 ya kuhamasisha uchanjaji kwa haraka utasaidia watu kuchanja kwa haraka zaidi kwani ugonjwa wenyewe unasambaa kwa haraka hivyo hakuna budi kwenda kwa haraka pia katika kukabiliana nao.
Kampeni hiyo itakuwa ya mtaa kwa mtaa kwa lengo la kutoa elimu kwa Jamii ili iweze kupata uwelewa zaidi na kufanya maamuzi ya hiari ya kuchanja.
Aidha, Dkt.Gwajima ametaja mikao inayofanya vizuri katika utoaji wa chanjo ni: Ruvuma,Mwanza,Dodoma, Kagera na Mara wakati Mikoa ya Manyara, Njombe, Singida, Iringa na Songwe hakufanya vizuri.
Mpango wa Serikali ni kuchanja kwa asimilia 60 ndipo Taifa litakuwa salama zaidi dhidi ya UVIKO 19, hayo yamesisitizwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi.
Amesema jumla ya watu 28218 walidhibitika kupata maambukizi ya UVIKO 19 na kati yao vifo vilikuwa 739 tokea wimbi la kwanza lilipoingia nchini.
Prof.Makubi amesema mpango huu wa uchanjaji wa awamu ya pili unalengo la kuhakikisha elimu inamilikiwa na wananchi wenyewe na wanaelimishana wenyewe katika Jamii zao.
Aidha, Katibu Mkuu TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe amewahimiza wananchi kuwalinda wazee waliopo Vijijini hasa kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka ili kupunguza vifo visivyo vya lazima.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe John Mongella amesema kwa niaba ya wakuu wa Mikoa yote kuwa wao kama wasimamizi wa Mikoa wapo tayari kulifanya hili zoezi liwe endelevu na lenye hamasa.
Pia, elimu hiyo watahakikisha inafika ngazi za chini kabisa kwani kwakufanya hivyo kutaokoa maisha ya watu na kuongeza kasi ya maendeleo kwa mtu mmoja hadi kwa nchi.
Uzinduzi wa mpango shirikishi na harakishi wa uchanjaji kwa awamu ya pili umefanyika baada ya mpango wa kwanza kuzinduliwa Jijini Dar es Salaam na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan mnamo mwezi Julai.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.