Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewataka watumishi wa hospitali ya Wilaya ya Arumeru hususani kitengo cha dharura waendelee kufanya kazi kwa kujitoa ili kunusuru uhai wa wananchi kwani wengi wanaofika pale wanakuwa mahututi.
Kauli hiyo ameitoa baada ya kufungua jengo la dharura katika hospitali ya wilaya ya Meru.
"Hospitali zinaitaji watu wenye uadilifu na nidhamu ya kazi kwasababu wanakuwa wameshikilia uhai wa wananchi wengi"alisema.
Watumishi wametakiwa kuongeza upendo na huruma kwa wagonjwa wanaoletwa katika kitengo hicho cha dharura.
Amesema kazi kubwa ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa karibu ndio maana fedha nyingi zimeletwa katika sekta ya afya ili kuendelea kuimarisha miundombinu yake.
Hali kadhalika Dkt. Mpango amewahasa wananchi wa Arumeru kuhakikisha wanatatua migogoro yao kwa amani na wakitaka kuishirikisha Serikali wafuate taratibu ili kuendelea kudumisha amani ya Mkoa.
Aidha, amewasisitiza TARURA kurekebisha barabara za Hospitali hiyo huku TAMISEMI wakiangalia kwa jicho la kipekee hospitali hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amesema barabara nyingi za wilaya ya Arumeru zinaitaji mitaro ya barabara kutokana na maeneo yake mengi kuwa juu kwenye Milima.
Amesema kwa uwekaji wa mitaro hiyo kutasaidia barabara zinazojengwa na Serikali kudumu kwa muda mrefu bila kuharibiwa na maji ya mvua.
Makamu wa Rais amelifungua jengo la dharura katika hospitali ya wilaya ya Meru ambalo limegharimu kiasi cha Milioni 800 ikiwemo uwekaji wa vifaa tiba katika jengo hilo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.