“Nendeni mkawe chachu ya kujenga amani na upendo miongoni mwenu na hata kwa nchi pia.”
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Idd Hassan Kimanta alipokuwa akifunga Mkutano wa 44 wa Kitaifa wa viongozi wa kanisa la wabaptist Tanzania, jijini Arusha.
Amesema kanisa lina mchango mkubwa sana wa kuleta amani, umoja na mshikamano miongoni mwao na nchi kwa ujumla kwani wao kama viongozi wa kanisa hilo wanahudumia waumini wengi.
Amewataka viongozi hao wakawe mstari wa mbele katika kulikuza kanisa hilo kwani yote waliyojadiliwa hapo ni maagano wameweka baina yao na mwenyezi Mungu.
Wajibu wao mkubwa ni kwenda kuwatumikia waumini wao lakini na Mungu pia.
Aidha, amesema serikali inatambua sana mchango unaotolewa na makanisa katika kujenga nchi hasa kwa kuleta amani na upendo miongoni mwa waumini.
Pia, amewashukuru viongozi hao kwa mchango mkubwa unaotolewa na kanisa hilo kwenye shughuli za maendeleo hasa kwenye sekta ya elimu na afya.
Nae, Baba askofu wa kanisa la Baptist Tanzania Arnold Manase Mollel, amesema kanisa hilo linatambua mchango na juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano na hivyo wataendelea kutoa ushirikiano katika kuleta maendeleo ya nchi.
Aidha, amesema kanisa hilo limekuwa likifundisha amani,upendo na mshikamano kwa waumini wake na litaendelea kufanya hivyo.
Mkutano huo umewakutanisha viongozi mbalimbali kutoka katika kanda zote 8 za kanisa hilo zilizopo nchini, na limetimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.