Wananchi wa kata ya Kansay wametakiwa kuilinda na kuitunza miradi ya maji waliyoletewa na serikali ili iwasaidie vizazi hadi vizazi.
Maelekezo hayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddi Hassan Kimanta alipokuwa akikagua na kuzindua miradi ya maji katika Kijiji cha Kansay na Kambi ya Faru, wilayani Karatu.
Amesema zaidi ya milioni 125 zimetolewa katika ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Kansay na milioni 15 katika Kijiji cha Faru ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika na kutoa maji.
Kimanta amesema, Serikali ya awamu ya tano inaendelea kuhakikisha inatekeleza kauli mbiu ya “Mtue mama ndoo ya maji” katika maeneo mengi ya nchi ikiwemo wilaya ya Karatu.
Mradi wa maji wa Kijiji cha Kansay utawafikia wananchi takribani 4768, shule 3 na kituo cha afya kimoja, wakati katika Kijiji cha kambi ya Faru mradi huo utawafikia wananchi takribani 3500, mifugo 2000 na shule 2.
Nae, kaimu mkuu wa kitengo cha wakala wa usambazaji maji na usafi na mazingira vijijini (RUWASA) wilaya ya Karatu Daudi Mwenduganga amesema,miradi hiyo ya maji imeweza kusaidia kupunguza magonjwa ya milipuko katika vijiji hivyo.
Pia, upatikanaji wa maji umeweza kusaidia kuokoa muda wa wanafunzi wengi katika kutafuta maji na badala yake wanautumia muda huo katika masomo yao.
Hali kadharika, faida ya miradi hiyo ya maji imewasaidia wamama kupata muda wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo ukilinganisha na kipindi cha nyuma walikuwa wanapoteza muda mwingi katika kutafuta maji kwa umbali umrefu takribani kilometa 6 hadi 8.
Mwenyekiti wa kamati ya maji Kijiji cha Kansay bi. Thekla Bayo na mwenyekiti wa Kijiji cha kambi ya Faru bwana Israeli Dafi wamesema, wameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuwaletea maji baada ya kuangaika zaidi ya miaka 7.
Wamesema wapo tayari kushirikiana na wanakijiji kuilinda na kuitunza miradi hiyo ili isiaribiwe.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, yupo katika ziara ya kikazi katika wilaya ya Karatu ambapo, amekagua miradi mbalimbali ikiwepo ukarabati na ujenzi wa miradi ya maji na hospitali, wilayani humo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.