Na Elinipa Lupembe
Uongozi wa Jiji la Arusha umetakiwa kuweka mkakati thabiti wa kuliweka Jiji hilo kwenye hadhi ya Jiji la Kimataifa kwa kuwa hapo ni kitovu cha utalii na uchumi wa mooa na Taifa la Tanzania.
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K. Mongella kwenye kikao kifupi cha maandalizi ya ziara ya siku mbili ya kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo, kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Arusha.
Mhe. Mongella licha ya kuwapongeza watalamu wa wilaya na Jiji la Arusha kwa kuanza kufanya kazi ya kuliweka Jiji hilo kwenye hadhi kwa kuanza kutekeleza mradi wa kuweka taa za barabarani, amewataka kuweka mpango mkakati wa kulifanya jiji hilo kuwa na hadhi ya Kimataifa.
Amesisitiza kutambua kuwa Jiji la Arusha ndio sura ya mkoa wa Arusha na ndio kitovu cha utalii, asilimia 80% utalii wa nchi, ni lazima uguse jiji la Arusha hivyo wanayo dhamana kubwa ya kulinda hadhi hiyo na kuifanya itambulike na kila mgeni anayeingia na kutoka Arusha.
"Mkurugenzi unawajibu wa kuhakikisha jiji linakuwa salama wakati wote, wananchi wanapata huduma stahiki na kuhakikishiwa usalama wao, kwa kuwa eneo hili ni nyeti sana kwa nchi yetu ikiwa ndio kitovu cha utaalii, wekeni taa barabara zote za jiji kwa awamu kadri mapato yanavyopatikana" Ameweka wazi
Aidha amewaelekeza Mkuu wa wilaya, Baraza la Madiwani, Mkurugenzi na watumishi wote, kutumia fursa hiyo adhimu kwa kuwa tofauti kuanzia utendaji kazi, mienendo, mipango na utekelezaji wa kasi, na kuonheza kuwa Jiji la Arusha linatakiwa kuwa mfano kwa halmashauri nyingine kwa kuwa limebeba wajibu mkubwa kama mtoto wa kiume wa kwanza katika mkoa wa Arusha.
"Hakuna asiyefahamu Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amerudisha heshima kubwa kwa Jiji na mkoa wa Arusha, ametupa hadhi ya kuonekana na kutambulika kitaifa na kimataifa, utendaji wake umelifungua Jiji letu,
baada ya Filam ya Tanzania Royo Tour kumetokea mlipuko mkubwa wa watalii ambao umesababisha kuwa na wageni wengi katika Jiji la Arusha na mkoa mzima wa Arusha, Arusha ndio kitovu cha Taasisi na jumuia zake zote za kikanda za Afrika, kwa sasa Taasisi nyingi zimakuja Arusha kwa shughuli mbalimbali pamoja na utalii" Amesema Mhe. Mongella
Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imefanya juhudi kubwa za kuifungua nchi, mkoa wa Arusha ukiwa umependelewa zaidi kwa kufungua fursa ambazo zilifungwa kwa kipindi cha nyuma, mikutano mingi ya kitaifa na kimataifa inafanyika Arusha.
Hata hivyo Mhe. Mongella amewapongeza waheshimiwa Madiwani kwa kutekeleza agizo la kuweka taa za barabarani, kwa sasa jiji limepata mwelekeo, kasi hiyo iendelee na kufikia lengo la kwa kutumia wakandarasi wenye bei za soko na kuwataka kuwahimiza wananchi kuchangamkia fursa kupitia wageni wanaoingia Arusha.
Awali mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John V.K. Mongella amezungumza na uongozi wa wilaya ya Arusha na wakuu wa Idara na vitengo Jiji la Arusha muda mchache kabla ya kuanza ziara ya kukagua shughuli za utekelezaji wa miradi ya maendeleo Jiji la Arusha.
#arushafursalukuki
#KaziInaendelea
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.