Na Daniel Gitaro
Wajumbe wa Kamati ya Lishe Mkoa wa Arusha wametakiwa kuongeza wigo wa kutoa elimu ya lishe, kwa jamii ili kupunguza idadi ya watoto wenye udumavu, changamoto inayojitokeza zaidi maeneo ya vijijini, katika mkoa huo.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Albano Mussa wakati akifungua kikao cha Lishe Mkoa wa Arusha robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa mkoa huo.
Mussa amesema kuwa, licha ya kuwa changamoto ya udumavu kwa watoto inaendelea kupungua siku hadi siku, bado kuna changamoto hiyo kwa watoto wa maeneo ya vijijini, inayochangiwa na uhaba wa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa lishe kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 2 na miezi 7 hivyo ni vyema wataalam kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kupanua wigo wa kuwafikia wananchi hao.
“Bado mkoa wetu unakabiliwa na changamoto ya utukelezaji wa afua za lishe kutonakana na sababu mbalimbali, hivyo niwatake wataalam kuongeza wigo katika kutoa elimu kwa jamii, zaidi tukachape kazi kwa bidii ili tuweze kukabiliana na changamoto hii ya udumavu kwa watoto”. Amesisitiza Katibu Tawala huyo.
Sambamba na hayo, amezitaka halmashauri zote za Mkoa huo, kuipa ajenda ya Lishe kipaumbele ikiwa ni pamoja na kupeleka fedha za kutekeleza afua za lishe kwa asilimia 100 kwenye maeneo yao kwa wakati, kama inavyoelekezwa kwenye bajeti zao.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Afua za lishe kwa kipindi hicho, Mratibu wa Lishe Mkoa wa Arusha, Doto Milembe, ameahidi kuendelea kupambana na udumavu kwa kuongeza wigo mikakati ya kuendelea kutoa elimu, hasa kwa kinamama wajawazito kupitia vikao mbalimbali, kliniki pamoja na mikutano inayoendeshwa kwenye ngazi ya jamii.
“Tunaendelea kuhamasisha akina mama na jamii yote kwa ujumla juu ya umuhimu wa ulaji wa makundi sita ya vyakula, ili kupata virutubisho vinavyopaswa kwa jamii na watoto pamoja na kuongeza idadi ya milo kwa watoto hadi kufikia milo 5, inayoshauriwa kwa siku”. Amesema Mratibu huyo.
Hata hivyo wadau walioshiriki kikao hicho, wameishukuru Serikali kwa mwamko mkubwa wa kuhimiza umuhimu wa lishe kwa jamii, pamoja na ushirikishwaji wa wadau jambo ambalo linarahisisha kuifikia jamii kwa pamoja kuliko kufanya kazi wenyewe.
Kwa upande wake Sheikh wa Wilaya ya Arusha, Shekhe Hussein Said Ijunje, ambaye amemuwakilisha sheikh wa mkoa huo, licha ya kuwapongeza wataalam kwa kazi wanayoifanya, ameshauri kuongeza nguvu zaidi na kuwafikia wananchi kwenye Kata, Vijiji na Vitongoji na kushirikisha viongozi wa dini, ambao wana ushawishi mkubwa kwenye jamii, kwa ajili ya kufikisha elimu hiyo na kupunguza kiwango cha udumavu kwa watoto wanaoishi maeneo ya vijijini ambapo tatizo ni kubwa kuliko maeneo ya mijini.
Awali, utekelezaji wa afua za lishe Mkoa wa Arusha, unakabiliwa na changamoto za ushiriki mdogo wa wanaume katika malezi, makuzi na lishe ya mtoto pamoja na upungufu wa vifaa vya kufanyia tathimini ya Lishe hususani vibao vya kupimia urefu kwa watoto chini ya miaka 5.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.