Wajumbe wa Kamati ya siasa mkoa wa Arusha, wametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu yenye kuishi familia mbili (2in1), shule ya sekondari Ayalabe, kata ya Ganako, halmashauri ya wilaya ya Karatu, ikiwa ni ziara ya kawaida ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025
Mwenyekiti amepongeza usimamizi mzuri wa mradi uliokamilika kwa viwango vya ubora unaoendana na thamani ya pesa huku wakibakiza fedha kiasi cha shilingi milioni sita.
"Tuwapongeze kwa ushirikiano ma kusimamia mradi vizuri, mradi ni mzuri unaonekana hata kwa macho, mmebakiza fedha za kufanya vitu vingine, lakini bado mna mipango mizuri ya kukamilisha miradi ambayo haijakamilika hapa, hongereni sana" Mwenyekiti Sabaya.
Diwani wa kata ya Kensay, amesema kuwa, kiasi hicho cha fedha kilichosalia kitatumika kukamilishia miradi viporo na kuongeza kuwa, tayari wameshaweka bajeti ya milioni 140 kukamilisha ujenzi wa majengo mengine viporo yaliyosalia shuleni hapo.
Ujenzi wa nyumba hizo za walimu umegharimu kiasi cha shilingi milioni 98, fedha kutoka Serikali Kuu, kupitia mradi wa kuboresha miundombinu ya shule za sekondari nchini (SEQUIP), nyumba ambayo tayari imekamilika na walimu wanaishi kwenye nyumba hiyo.
Lengo la mradi huo ni kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzi kwa walimu na wanafunzi kwa kuwawezesha walimu kuishi ndani ya eneo la shule, kwa kuwapunguzia umbali wankutembea pamoja na gharama za kulipa kodi ya nyumba nje ya eneo la shule.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.