Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ameitaja sekta ya ardhi kuwa kinara katika vitendo vya rushwa mkoani Arusha na kuahidi kushirikiana na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa katika kuhakikishwa kuwa rushwa haiwi sababu ya wakazi wa Arusha kukosa haki zao.
Mhe. Makonda ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Septemba 13, 2024 wakati alipotembelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Chrispin Francis Chalamila aliyefika ofisini kwa Mkuu wa mkoa kujitambulisha na kumpongeza kwa kuwa kinara katika mapambano dhidi ya rushwa mkoani Arusha.
"Tutahakikisha kuwa upande wetu hakuna jambo linalokwamisha vijana wako kufanya kazi yao kikamilifu. Sisi tunachotaka ni haki, mtu asionewe na watu wasiishi kwa mazoea kwamba bila rushwa hauwezi kufanikisha jambo lako. Tunatamani mkoa wetu huu utawaliwe na Mungu kwa maana kwamba haki ndiyo iwe msingi wa kila mtu" Amesema Mhe. Makonda.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ameahidi kuongeza maafisa zaidi mkoani Arusha kabla ya mwezi Novemba mwaka huu ili kuongeza kasi katika mapambano dhidi ya rushwa, ikiwa ni utekelezaji wa ombi la Mhe. Makonda alilolitoa kwa TAKUKURU Mwezi Mei mwaka 2024.
Aidha Chalamila amemuomba Mhe. Mkuu wa Mkoa kusimamia kikamilifu uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu, akisema kuwa kupatikana kwa viongozi sahihi na wasiojihusisha na rushwa ni sehemu ya kuharakisha maendeleo ya mkoa wa Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.