Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amewahamasisha wasichana na wanawake kuchangamkia fursa ya kuwa waongoza watalii Mkoani Arusha, kutokana na kusifika kwao kwa utulivu, busara na sifa nyingine za asili wawapo barabarani na namna ambavyo wamegeuka kuwa kivutio kwa watalii mbalimbali ambao mara zote hueleza kufurahia kuhudumiwa na kuendeshwa safarini na wanawake.
Leo Machi 04, 2025, akizungumza wakati akiwa anaendeshwa na Muongoza watalii Bi. Tumaini Paul Sayala maarufu kama Hope, Mhe. Makonda amesema kuongozwa na mwanamke kunaongeza utulivu kutokana na umakini alionao mwanamke suala ambalo limesababisha mara zote wanawake kuhusika na ajali chache, ambazo mara kadhaa zikiwa ni za kusababishiwa wawapo barabarani.
"Mwanamke kwenye gari la utalii anaongeza kivutio cha pili kwa mtalii, namna wanavyoweza kueleza mambo hasa pale mwanamke anapoamua kukueleza kitu, wamekuwa wataalamu kabisa katika hilo. Nihamasishe watoto wa kike kujitokeza kwa wingi, msisite njooni Arusha kuchangamkia fursa hii muhimu." Amesema Mhe. Makonda.
Kwa upande wake Muongoza watalii huyo, ameeleza kufurahishwa na maandalizi na shamrashamra za siku ya mwanamke duniani kwa mwaka huu, akikiri kuwa ni kwa mara ya kwanza anashuhudia shamrashamra zenye kuhusisha sekta mbalimbali wakati huu Arusha ikiwa mwenyeji wa siku ya wanawake Kitaifa, Mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan hapo Machi 08, 2025.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.