NGORONGORO:
Kundi la pili lenye kaya 11 na wananchi 43 pamoja na mifugo 36 waliokuwa wamejiandikisha kuhama kwa hiari wameagwa leo tarehe 19 Oktoba, 2023 na kuhamia katika maeneo waliyoyachagua katika Wilaya za Monduli, Meatu, Arusha vijijini, Simanjiro na Handeni ambayo wameyachagua.
Akiwaaga wananchi hao kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Raymond Mwangala amesema hatua hiyo ni muendelezo wa awamu ya pili ambapo kundi la kwanza lilihama tarehe 24/8/2023 ambapo jumla ya kaya 16 zenye watu 87 na mifugo 733 zilihamia Wilaya za Monduli, Karatu, Meatu na Arusha.
Mwangala ameongeza kuwa katika utekelezaji wa zoezi hilo wananchi wanaojiandikisha wanapata fursa ya kuchagua maeneo yaliyopangwa na Serikali na maeneo mengine ambayo watachagua wenyewe na Serikali itawalipa fidia na stahiki zao kwa mujibu wa Sheria.
“Zoezi hili linafanyika kwa kufuata sheria zote za nchi, utu, na haki za binaadamu, tumepanua wigo zaidi ambapo pamoja na maeneo yaliyotengwa na Serikali mwananchi ana haki ya kuchagua popote anapotaka kwenda na Serikali itampa staki zake kwa mujibu wa sheria”,alisema Mhe.Mwangala
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa kuhamisha watu awamu ya Pili Kamishna Msaidizi mwandamizi Mdala Fedes amebainisha kuwa Serikali imeongeza idadi ya nyumba zinazojengwa kutoka 503 za awamu ya kwanza hadi kufikia nyumba 5,000 katika awamu ya pili na kuongeza idadi ya huduma za kijimii kama vile maji, shule, vituo vya afya, umeme , barabara, mawasiliano na huduma za mifugo na posta.
Ameongeza kuwa mradi wa ujenzi wa Nyumba umepanuka katika maeneo mengine ya Mkoa wa Manyara na Wilaya ya Kilindi na Handeni ambapo nyumba 1500 zinatarajiwa kujengwa katika kijiji cha Kitwai B kilichoko Wilaya ya Simanjiro, nyumba 1,000 kijiji cha Saunyi kilichopo Wilaya ya Kilindi Mkoa wa Tanga na nyumba zingine 2500 zitajengwa katika kijiji cha Msomera kilichoko Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga.
Tangu zoezi la wananchi waliojiandikisha kuhama kwa hiari lilivyoanza hadi kufikia tarehe 18.01. 2023 jumla ya kaya 551 zenye watu 3,010 na mifugo 15,321 zimehamia katika kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga lengo likiwa ni kuboresha huduma za kijamii za wananchi hao na kulinda Hifadhi ya Ngorongoro
Chanzo.
Na Kassim Nyaki, Karatu
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.