Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS) kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta, wadau na jamii kwa ujumla kuweka mkazo katika kudhibiti mazingira yanayochochea maambukizi ya UKIMWI.
Makamu wa Rais ametoa rai hiyo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika Kitaifa Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma. Aidha, ametoa wito kwa vijana kujitambua, kujithamini na kutunza maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa kuwa kasi ya maambukizi katika kundi la vijana bado inaonekana kuwa kubwa ambapo takwimu za hali ya UKIMWI nchini zinaonesha kundi la vijana na hasa wa kike liko kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi mapya ya VVU.
Makamu wa Rais amewasihi wananchi kuzingatia maudhui ya elimu inayotolewa kupitia kampeni mbalimbali kwa ajili ya kubadili tabia, kuachana na mila zinazoweza kuwa vichocheo vya maambukizi na kuendelea kujikinga na maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI. Amesema hali ya maambukizi mapya inaonekana kuchochewa zaidi na mazingira na tabia hatarishi hususan ulevi uliopindukia, ngono zembe, kuwa na wapenzi wengi na matumizi ya dawa za kulevya.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuondoa mtazamo hasi uliopo juu ya walioathirika ambao huchangia kurudisha nyuma jitihada za kupambana na UKIMWI. Amesema mtazamo hasi huwafanya wahitaji kushindwa kupata huduma kwa kuonekana kuwa hawastahili na hivyo kutengwa. Ameongeza kwamba unyanyapaa hupelekea woga unaoathiri upimaji kwa hiari na upatikanaji wa huduma nyingine kama za unasihi pamoja na ARV kwa wale wanaoishi na VVU.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inaendelea kutekeleza awamu ya tatu ya Mradi wa TIMIZA MALENGO ambao unaolenga Wasichana Balehe na Wanawake Vijana, wenye lengo la kuwasaidia kiuchumi na kijamii, ili kupunguza hatari na kuhakikisha wanabaki salama dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI mradi huu unatekelezwa katika Halmashauri 42”.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.