Mbunge wa Arumeru Magharibi Mhe. Noa Lembris, akizungumza kwenye Mafunzo ya Usambazaji na Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 kwa viongozi wa makundi mbalimbali ya kijamii, mkoa wa Arusha, yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa AIM MALL Jijini Arusha leo tarehe 11 Desemba, 2023.
Mhe. Noa licha ya kuwapongeza watalamu wa Ofisi ya Takwimu nchini, kwa kuweza kufanikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi na hatimaye kuja na matokeo ambayo bado wameona umuhimu wa kuhakiksiha wananchi wanayafahamu na namna ya kuztumia takwimu hizo.
Ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita kuona umuhimu wa kufanya Sensa ya watu na makazi, ili kuwa na mipango sahihi inayoendana na Idadi ya watu, makazi pamoja na rasilimali zilizopo, jambo ambalo litarahisisha katika upangaji wa shughuli za maendeleo ya jamii na kufikia malengo ya Serikali.
"Serikali ya awamu ya sita licha yakufanya tukio muhimu la Sensa bado imewekeza fedha nyingi kwenye ujenzi wa miundombinu katika sekta zote, na kuwafanya wananchi kuapta huduma karibu na maeneo yao, tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulipendelea Jimbo la Arumeru Magharibi, miradi iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya sita haijawahi kutokea, tunamshukuru sana kwa niaba ya wananchi wa halmashauri ya Arusha na vitongoji vyake" Amesisitiza Mhe. Noah
Mkutano huo umefunguliwa na Katibu Tawala Msaidizi Utumishi na Rasilimali Watu, mkoa wa Arusha, David Lyamongi kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Arusha, ukiwa na lengo la kuyajengea uwezo makundi mbalimbali ya kijamii juu ya matumizi sahihi ya matokeo ya Sensa ya watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022.
Makundi hayo ni pamoja na viongozi wawakilishi wa wananchi, viongozi wa Siasa, dini na mila, Watendaji wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, watendaji wa kata, kamati ya Sensa Mkoa pamoja na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo watu wenye mahitaji maalum.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.