Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufungua jukwaa la kodi na uwekezaji la mwaka litakalo fanyika Jijini Dar es salaam mwezi Februari,2024, lenye lengo kukusanya maoni kutoka kwa wadau na wananchi ili kusaidia kuandaa bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2024/2025.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, kwenye ofisi za Hazina ndogo Jijini Arusha, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya amesema kuwa, Kongamano hilo litakalokutanisha zaidi ya wadau 800 , wakiwemo wafanyabiashara, mabalozi, wadau wa sekta binafsi wa ndani na nje ya nchi, ikiwa ni utaratibu wa kawaida wa utoaji wa maoni yao kwa ajili ya kuandaa bajeti ya mwaka wa fedha unaofuata.
Mwandubya, ameyataja malengo ya jukwaa hilo ni pamoja na kuangalia mustakabali wa ulipaji wa kodi, hali ya uchumi na uchumi jumuishi, kuangalia wafanyabiashara wapya na kuwa na utaratibu imara wa kuziwezesha biashara zao kukua na kuongeza kuwa, tayari wameshakusanya maoni kwenye Kanda mbalimbali nchini, na Februari 27 na 28 itakua ni kilele cha kukusanya maoni hayo." Amesema.
Hata hivyo, ameweka wazi kuwa, tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo, kumekuwa na mafanikio makubwa, ikiwemo ukusanyaji mzuri wa mapato, ambapo kwa kipindi cha mwezi Disemba mwaka 2023, serikali ilikusanya shilingi Trilioni sawa na 12%.
Ameongeza kuwa, licha ya mafanikio hayo, bado kuna changamoto mpya zinazojitokeza na wizara inazitafutia ufumbuzi, ikiwa ni sehemu ya majukumu yao ya kuongeza na kuchochea ufanisi, katika kipindi cha maboresho ya kukuza uchumi wa Taifa, na kuhakikisha pato la Taifa linakua.
"Maboresho yanayoendelea ni pamoja na msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwa uuzaji wa nyumba mpya zisizozidi thamani ya shilingi milioni 50, pamoja na vifaa vinavyobadili magari kutoka kwenye mafuta kwenda kwenye gesi, kuongeza ushindani kwa kuwasajili wafanyabiashara wenye mitaji ya shilingi milioni 200 kwenye mfumo wa ulipaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT)" Amebainisha Mwandumbya
Awali, jukwaa hilo lilifanyika Kitaifa kwa mara ya kwanza Januari 11, 2023 Jijini Dar es Salaam , maoni yaliyopokelewa yalisaidia kuandaa bajeti ya Serikali, inayotekelezwa mwaka wa fedha 2023/2024
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.