Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amewataka wakandarasi waliosaini mikataba ya kutengeneza Barabara wakafanye kazi kwa weledi, uzalendo na kuzikamilisha kwa muda uliopangwa.
Ameyasema hayo alipokuwa akishuhudia utiaji saini wa mikataba kati ya Wakala wa barabara vijijini na Mijini ( TARURA) na wakandarasi takribani 18 kwa Mkoa wa Arusha.
Katika hatua hiyo ya kusaini mikataba Mongella amewataka wakandarasi hao wakafanye kazi zenye viwango.
Amesema,kwa kukamilisha barabara hizo kwa wakati na kwa viwango kutasaidia kushusha gharama za maisha kwa wananchi.
Aidha, amewaelekeza TARURA wakawasimamie wakandarasi hao kwa ukaribu zaidi ili wakamilishe miradi hiyo kwa wakati.
Pia, amewataka wakasimamie miradi ya barabara ya zamani ili nayo iweze kukamilika haraka.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Missaile Musa amesema, kwa kitendo cha wakandarasi kusaini mikataba hadharani kitasaidia wananchi kuwafahamu wakandarasi watakaoenda kufanya kazi katika maeneo yao.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha Lynas Sanya amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 walipatiwa jumla ya fedha za matengenezo ya barabara zaidi ya bilioni 18 kwa awamu ya pili na katika awamu ya kwanza mikataba 34 ilisainiwa yenye thamani ya bilioni 14 sawa na 60%.
Awamu ya pili ya utiaji saini umewekwa katika mikataba 18 yenye thamani zaidi ya bilioni 4.07 sawa na 40%.
Amesema,kwa mwaka wa fedha 2022/2023 TARURA katika bajeti yake wamepatiwa zaidi ya bilioni 10 fedha zilizotokana na tozo za mafuta ili zikasaidie katika ukarabati wa barabara katika Mkoa wa Arusha.
Nae, Mkandarasi Rashidi Sevingi kutoka kampuni ya Raly (EA) Limited amewahasa wakandarasi wengine kwenda kutekeleza mikataba waliyosaini kwa weledi ili waendelee kuaminiwa zaidi na Serikali.
TARURA kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wamesaini Mikataba 52 yenye thamani ya bilioni 18 kwa ajili ya ukarabati wa barabara mbalimbali za Mkoa wa Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.