Katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Jemadari Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoa wa Arusha umejipanga kusimamia vema utekelezaji wa mchakato wa Ununuzi wa Umma kupitia mfumo wa kidijitali wa NeST.
Hayo yamewekwa wazi na Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhe. Amir Mohamed Mkalipa, wakati akimkaribisha mgeni rasmi na Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Mchemba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, ili afunge Jukwaa la 16 la Ununuzi wa Umma Nchi wa Jumuia ya Afrika Mashariki, lililofanyika kwa siku 4 mkoani Arusha, kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha - ICC, ukumbi wa Simba, leo Septemba 12, 2024.
Mhe. Mkalipa amemuahidi Waziri wa Fedha kuwa, Uongozi wa Mkoa wa Arusha utasimamia matumizi sahihi ya mfumo wa NeST kwa Mamlaka za Serikali za mitaa, Mashirika ya Umma na Taasisi zote za Serikali mkoani Arusha ili kuongeza tija na ufanisi ikiwa ni mkakati wa kufikia malengo ya Serikali ya matumizi sahihi ya fedha za Umaa kupitia Ununuzi.
"Nitumie fursa hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa umuhimu sekta ya ununuzi wa Umma, kama mkoa tunaahdi kusimamia vema manunuzi yote ya fedha za Umma kutumia mfumo wa NeST" Amebainisha Mhe. Mkalipa
Amesema kubwa, Taasisi za Serikali zimeshuhudia maboresho makubwa katika michakato ya ununuzi, ambapo matumizi ya mifumo ya kidijitali kama mfumo wa ununuzi wa NeST, imeanza kusomana na mifumo mingine ya Taasisi za Serikali na kuleta ufanisi mkubwa kwenye mchakato wa Ununuzi wa Umma.
Hata hivyo, kwa niaba ya wananchi wa mkoa huo Mhe. Mkalipa amewapongeza na kuwashukuru waandaaji wa Jukwaa hilo wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma Denisi Simba kwa kuchagua Arusha kuwa sehemu ya kufanyika mkutano huo mkubwa wa Kitaifa, jambo linaloendelea kuchochea uchumi wa mkoa huo kupitia sekta ya Utalii,hususani Utalii wa Mikutano.
"Jukwaa hili limeunga mkono juhudi za Uongozi wa mkoa wetu za kukuza shughuli za utalii ikiwamo utalii wa Mikutano, kwa kuzingatia Arusha ni kitovu cha Utalii"
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.