Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K. Mongella, ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuboresha hali ya upatikanaji huduma rasmi za kifedha, huku akithibittisha, wananchi wa mkoa huo, kunufaika kwa kutumia huduma hizo, kwa maendeleo ya uchumi wa mtu mmoja mmoja, mkoa na Taifa.
Mhe. Mongella amesema hayo, akitoa salamu za mkoa, muda mfupi kabla ya Ufunguzi wa, Maadhimisho ya 3 ya Wiki ya Huduma za Kifedha, yanayofanyika mkoani Arusha, kwenye viwanja vya Sheik Amri Abeid, Jijini Arusha.
Amesema kuwa, Arusha ni miongoni mwa mikoa mitano ya mwanzo, inayofanya vizuri katika Sekta ya Fedha nchini, kwa mujibu wa utafiti wa Finscope wa mwaka 2023, utafiti unaonyesha, hali ya upatikanaji wa Huduma Jumuishi za Fedha, ukiongezeka na kufikia 82.2% mwaka 2023, kutoka 74% mwaka 2017, huku upatikanaji na utumiaji wa huduma kifedha kupitia Benki, ukiongezeka pia na kufikia 34% kutoka 29%.
"Kumekuwa na ongezeko pia, katika sekta ndogo za bima, Masoko ya Mitaji na Dhamana, hifadhi ya jamii na huduma ndogo za fedha, na kufikia 48% kutoka 45%, jambo ambalo linaimarisha uchumi wa wananchi, kuboresha kipato pamoja na kuboresha hali ya maisha ya kaya za wakazi wa Arusha" Amethibitisha Mhe. Mongella
Licha ya mafanikio hayo, ameweka wazi kuwa, bado kuna changamoto ya utumiaji wa huduma za fedha zisizo rasmi licha ya kupungua kufikia 3% mwaka 2023 kutoka 5% mwaka 2017 na kuzisisitiza Taasisi za Fedha kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kufahamu madhara ya kutumia hufuma zisizorasmi ambazo zina matokeo hatarishi.
Ameyataja mafaniko mengine makubwa katika mkoa huo, ni kupungua kwa kiwango cha watu wazima wasiotumia huduma za fedha, kutoka a 21% mwaka 2017 na 15 % mwaka 2023.
Aidha, Mhe. Mongella amebainisha kuwa, Arusha ni miongoni mwa mikoa yenye fursa nyingi za kiuchumi kisekta ikiwemo Utalii, Kilimo, Ufugaji na Madini, ambapo ukuaji na uzalishaji wa sekta hizi unategemea sana uwepo wa Sekta ya Fedha endelevu na imara.
"Ninawashukuru wasimamizi wa Sekta ya Fedha nchini, kwa jitihada za kusimamia sekta hii muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu, uwepo wa Sheria na Miongozo madhubuti, zimeendelea kupunguza migogoro ya masuala ya kifedha licha ya kuwa bado wananchi wanakabiliwa na changamoto za uelewa mdogo na kujiingiza kwenye mikopo umiza kama 'Kausha damu' huku baadhi yao, wakopeshaji binafsi na Vikundi vya Kijamii bila ya kusajiluwa wala kuwa na leseni.
Awali, Mhe. Mongella amewashukuru waandaaji kwa kuteuliwa kuandaa na kushiriki Maadhimisho ya tatu ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kwa mwaka 2023 yenye kauli mbiu ‘Elimu ya Fedha ni Msingi ya Maendeleo ya Kiuchumi’’
#ArushaFursaLukuki
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.