Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania limemsimamisha kazi kwa muda wa mwaka mmoja Muuguzi Msaidizi daraja la kwanza kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mt. Meru Bwana Martini Joseph Chamani kwa kwenda kinyume na maadili ya kazi yake ya uuguzi.
Akisoma hukumu hiyo mwenyekiti wa baraza hilo Bwana Abner Mathube amesema, maamuzi hayo ya baraza yamefikiwa baada ya kusikiliza upande wa mtuhumiwa, mashaidi na mlalamikaji na baraza likaridhishwa na maelezo ya pande zote na kuona kuwa kuna ukiukwaji wa maadili ya kiutendaji kwa muuguzi hiyo.
Abner amesema, Bwana Martini amekutwa na hatia kwa kosa la kuchelewa kuingia kazini na kutumia kilevi wakati wa kazi na kupelekea kushindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo.
Aidha, Bwana Abner ametoa rai kwa wauuguzi na wakunga wote nchini kuhakikisha wanafuata maadili ya kazi zao na kuzingatia sheria ili kuepusha migogoro na adhabu kama hizo kutokea mara kwa mara.
Amesema bado mtuhumiwa bwana Martin ana nafasi ya kukata rufaa dhidi ya adhabu hiyo aliyopatiwa na baraza hilo.
Nae Msajili kutoka Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania Bi.Agnes Mtawa anasema kazi kubwa ya baraza ni kuwasajili na kuwasimamia wauguzi na wakunga nchini katika kazi zao, na katika kazi wanaangalia pia nidhamu zao.
Amesema baraza linapoletewa malalamiko juu ya Muuguzi au Mkunga huwa linafuatilia mambo aliyoyafanya na ikithibitika mambo aliyoyafanya ni kinyume na sheria linatoa adhabu, na kwa mujibu wa sheria ya baraza adhabu zipo za aina tatu; Kumfukuza na kumfuta kwenye dafturi la usajali,kumsimamisha kutoa huduma za uuguzi na ukunga kwa kipindi ambacho baraza litaamua na kutoa kalipio kali.
Kwa shauri hili la Bwana Martin kulingana na taratibu za baraza atatakiwa kurudisha leseni ya uuguzi na vyeti vya usajili na atakapokamilisha adhabu yake atarudishiwa. Anapokuwa nje ya huduma za uuguzi baraza litaendelea kumfuatilia kwa karibu na ikithibitika atafanya matenda kinyume na taratibu ikiwemo kutoa huduma za uuguzi na ukunga wakati amesimamishwa kazi atafutiwa kabisa usajili wake.
Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania limefanya kikao chake cha 196 Mkoani Arusha na moja ya agenda ilikuwa kusikiliza mashitaka dhidi ya muuguzi Bwana Martin kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mt.Meru.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.