Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amewaambia wananchi wa Mkoa wa Arusha kuwa nafasi na Cheo chake na nguvu zake zote amezielekeza kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha wanaojihisi kusahaulika na kutotendewa haki na watumishi wasiokuwa waaminifu na wananchi wenye fedha.
Mhe. Makonda ametoa kauli hiyo leo Mei 09, 2024 Ofisini kwake, ikiwa ni siku ya pili ya Kliniki ya Haki Mkoa wa Arusha inayolenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi akisema kuwa amefarijika kwa matumaini na wingi wa wananchi waliojitokeza ofisini kwake licha ya mvua kubwa kunyesha tangu majira ya asubuhi.
Akizungumza na Mamia ya wananchi kwenye Viwanja vya Makao makuu ya Mkoa, Mhe. Makonda ameahidi kutunza na kutekeleza kikamilifu tamanio la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan la kukataa dhulma na kuminywa kwa haki za wananchi hasa wananchi walio wanyonge.
Hata hivyo, amewataka watendaji na watumishi wa ofisi yake wanaosikiliza wananchi pamoja na Mawakili wanaotoa msaada wa kisheria kwa wananchi kuongeza kasi katika kuhudumia wananchi ili kuhakikisha wananchi wote wanasikilizwa na kutatuliwa changamoto walizonazo.
Katika Hatua nyingine Mhe. Makonda ameonesha kushangazwa na baadhi ya watu wanaotumia mitandao kukosoa Kliniki hiyo ya kuwasikiliza wananchi na kusema kuwa nafasi yake siku zote ataitumia kwaajili ya kuhakikisha wananchi wananufaika kuaminika kwake na mteule wake ambaye ni Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyemuamini na kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.