Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli leo ameweka jiwe la msingi katika mradi wa maji safi na usafi wa mazingira wa jijini Arusha katika kata ya Kimnyaki wilayani Arumeru.
Amesema wananchi wote ambao wanaishi katika vyanzo vya maji na ambao mradi utawapitia katika maeneo yao watapatiwa maji kwanza wao kabla yakusambazwa maeneo mengine.
Magufuli amesema mradi huu ambao utawanufaisha wananchi wa jiji la Arusha kwa kiasi kikubwa lakini hata pia wananchi wa kata ya Oldonyosambu wilayani Longido pia nao wapatiwe maji kutoka kwenye mradi huo.
“Jana nimesimamishwa njiani na wananchi wa Oldonyosambu na kero yao kubwa ilikuwa ni ukosefu wa maji safi kwani wanayoyatumia sasa yama madini ya Floride kwa wingi hivyo yanawaadhiri sana wao na watoto wao.”
Amesema fedha zilitumika katika ujenzi wa mradi huo wa maji ni mkopo wa riba nafuu kutoka Benk ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), hivyo wananchi wote wanajukumu la kulilipa deni hilo.
Magufuli amewataka wakandarasi wa mradi huo ambao wapo 10 wafanye kazi kwa bidii usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika ifikapo mwanzoni mwa Juni 2020 na wananchi waweze kupata maji kwa haraka.
Waziri wa maji na umwagiliaji Pro Makame Mbalawa amesema, hitaji la maji kwa mkao wa Arusha ni lita milioni 94 kwa siku lakini mradi huo unauwezo wakuzalisha lita milioni 208 kwa siku hivyo ni zaidi ya mara 4 ya uhitaji wa Mkoa.
Akisoma taarifa ya mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na taka Arusha Enginia Ruth Koya amesema, mradi huo hadi kukamilika utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 520.
Amesema mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 208 kwa siku tofauti na hali ya sasa ambayo ni lita milioni 40 kwa siku huzalishwa sawa na asilimia 42 na hitaji la mkoa ni lita milioni 94 kwa siku.
Koya amesema kutokana na ongezeko hilo la uhitaji wa maji wa takribani asilimia 100 hadi ifikapo 2020 mkoa wa Arusha utakuwa na uwezo wakuwahudumia watu takribani milioni 1.
Mbali na mafanikio hayo amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni ugumu wa kupata njia zakulaza mabomba hasa katika maeneo ambayo hayajapimwa,pia gharama kubwa za fidia wanazopaswa kuwalipa wananchi.
Rais Magufuli amefanya ziara yake katika mkoa wa Arusha kwa siku 2 kuanzia Desemba 1 hadi Desemba 2,2018 nakuweza kufungua kituo cha malipo ya forodha cha pamoja Namanga wilayani Longido na kumalizia na uwekaji jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa maji safi na mazingira wa jijini Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.