Na Elinipa Lupembe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mapema leo Juni 24, 2024 amepiga simu mubashara na kuzungumza na Maelfu ya wakazi wa Arusha walioitikia na kuhudhuria siku ya kwanza ya Kambi maalum ya Madaktari bingwa wanaotoa huduma za matibabu bure kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha.
Rais Samia kwenye mazungumzo yake amempongeza Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda kwa kuandaa kambi hiyo, akiwashukuru Madaktari na watoa huduma zaidi ya 450 waliojitolea kupima, kushauri na kutoa matibabu ya bure kwa kila mwananchi atakaehudhuria kwenye kambi hiyo inayofanyika kwenye viwanja vya michezo vya kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid.
" Serikali kuu itaangalia nini cha kuwekeza hapo ili kuunga mkono jitihada za mkoa ili wananchi wapate matibabu. Nakushukuru wewe (RC Makonda) na kamati yako kwa kuliwaza hilo kwani kwasababu hiyo sasa Kambi hiyo inawarahisishia wananchi kupata matibabu mahali pamoja", Ameongeza Rais Samia.
Rais Dkt. Samia ametumia nafasi hiyo pia kuwapa pole wananchi wote wenye kusumbuliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya akiahidi kuendelea kuboresha huduma za afya ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana za uhakika na zenye kukidhi mahitaji ya wananchi.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.