Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Jseshi la Polisi kumkata na kumchunguza Afisa Mtendaji wa kata ya Bwawani, Simon Kaaya, kwa tuhuma za kulalamikiwa na wananchi kuuza shamba la kijiji na kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi kwenye kata hiyo,
Mhe. Paul Christian Makonda amefikia hatua hiyo leo Mei 28, 2024 wakati akiendelea na ziara yake Wilayani Arumeru ambapo wananchi wa Kata ya Bwawani wamemlalamikia Afisa Mtendaji huyo, akidaiwa kuwa ndiye sababu ya migogoro ya ardhi kwa kuuza ardhi ya Kata hiyo kwa watu mbalimbali.
Hata hivyo, Mhe. Makonda amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Arusha kumfanya uchunguzi wa tuhuma zilizowasilishwa na wananchi dhidi ya Afisa Mtendaji na kutoa taarifa.
Katika Mkutano huo, Mwananchi wa kijiji cha Bwawani Lucas Samwel amemuelezea Mkuu wa Mkoa kuwa Mtendaji huyo amemsababishia hasara kubwa ya kifedha kutokana na kukopa fedha zaidi ya Milioni sita kwaajili ya kununua shamba alilouziwa na Mtendaji huyo na wakati Mtendaji huyo aliposikia Ujio wa Mkuu wa Mkoa alimuita Bw. Lucas na kutaka kumrejeshea Milioni tatu kati ya milioni sita ikiwa ni miaka miwili baadae.
Mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, imedaiwa kuwa Afisa Mtendaji huyo amekuwa akiwatafuta watu na kuwafanya kuwa wamiliki wa ardhi ya kata na baadae Mtu huyo kuanza kuuza ardhi hiyo ikiwa ni kinyume na sheria na taratibu za ardhi.
Awali, akiwasilisha taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Mhe. Emmanuela Kaganda alimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa, wilaya ya Arumeru miongoni mwa Wilaya sita za Mkoa wa Arusha inaongoza kwa migogoro ya ardhi na hivyo kumuomba Mkuu wa Mkoa kutoa usaidizi katika kutokomeza migogoro hiyo ya ardhi iliyodumu kwa miaka mingi.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.