Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amemuomba Mhe.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuiunganisha Zanzibar na Mkoa wa Arusha kwenye sekta ya utalii ili kuwezesha mabadilishano ya Watalii wa pande hizo mbili.
Mhe. Makonda pia amemuomba Mhe. Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi kutangaza fursa na vivutio vya Uwekezaji vilivyo Mkoani Arusha katika adhma ya kutimiza maelekezo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza vyumba na Vitanda vya kulala wageni mkoani Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha ametoa maombi hayo mbele ya Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye leo ndiye mgeni rasmi kwenye Semina maalum ya wanahisa wa Benki ya CRDB, semina inayofanyika kwenye Kituo cha kimataifa cha Mikutano mjini Arusha - AICC.
Katika hatua nyingine Mhe. Mkuu wa mkoa ameishukuru benki ya CRDB kwa kuwa mdau mkubwa wq maendeleo ya Mkoa wa Arusha pamoja na kuichagua Arusha kuwa Mwenyeji wa semina ya wanahisa na Mkutano Mkuu wa 29 wa wanahisa unaotarajiwa kufanyika Mei 18, 2024 Jijini Arusha.
Katika majibu yake Mhe. Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi amemuahidi Mhe. Mkuu wa Mkoa kuwa atatetekeleza maombi yake ipasavyo hasa katika suala la uwekezaji wa ujenzi wa hoteli na nyumba za kulala wageni kutokana na idadi kubwa ya Wawekezaji wanaofika Zanzibar kutaka kuwekeza kwenye ujenzi wa nyumba na vyumba vya kulala wageni na watalii wanaofika nchini.
Akiapishwa mwishoni mwa Mwezi Machi Mwaka Huu, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan alimuagiza Mkuu wa mkoa wa Arusha kupambana katika kukuza utalii wa Arusha pamoja na kuongeza idadi ya vyumba na vitanda vya kulala wageni na watalii kutokana na upungufu mkubwa unaokadiriwa kutokea kutokana na matokeo chanya ya filamu ya The Royal Tour iliyokuwa na nia ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini Tanzania ikiwemo vile vilivyopo mkoani Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.