Na Elinipa Lupembe
MKuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda amepiga marufuku tabia ya wahudumu wa afya katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya Arusha, kuzuia mwili wa marehemu kwa sababu ya ndugu kukosa pesa ya kulipa bili alizokuwa anadaiwa marehemu alipokuwa anatibiwa.
Mhe. Makonda ametoa marufuku hiyo, wakati akizungumza na wahudumu wa afya wa hospitali ya Wilaya ya Monduli, alipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya hospitali hiyo, leo Mei 28, 2024.
"Ni marufuku kwa wauguzi wote Mkoa wa Arusha, kung'ang'ania mwili wa mgonjwa aliyepoteza maisha kwa sababu ndugu zake hawana uwezo wa kulipa matibu aliyotumia wakati akiwa mgonjwa" Amesisitiza Mhe.Makonda
Aidha, ameweka wazi kuwa, kazi ya kutoa huduma ya afya sio kazi nyepesi bali kazi nzito inayohitaji hekima ya hali ya juu kwa kuwa, kazi hiyo ni mpango wa Mungu wenye lengo la kuokoa maisha ya watu na kufafanua kuwa, wananchi wanaokuja hospitali wanahitaji kupata faraja ya maneno mazuri yanayoashiria uponyaji kutoka kwa wauguzi.
"Tunapaswa kutambua, huduma ya utabibu ni ya pekee ambayo mtu anaweza kumuona Mungu na usiwe sehemu ya kumuonesha mgonjwa kuwa huponi lakini tunzeni siri za wagonjwa na kuwahudumia, wanapofika kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya iwe sehemu ya faraja na uponyaji, wagonjwa wajisikie fahari kuhudumiwa katika hospitali zetu za Serikali" Amesema Mhe.Makonda.
Ameongeza kuwa licha ya changamoto zinazoikabili sekta ya afya ni vema watabibu wa Mkoa huo, kuwahudumia wagonjwa wakiwa na tabasamu na kwa upendo, na kuwa mfano bora kwa wauguzi wengine, ili kuenzi heshima ya viongozi waasisi wa hapa Monduli Hayati Edward Lowasa na Edward Sokoine.
Hata hivyo, Mhe. Makonda ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo fedha za upanuzi wa majengo muhimu kwenye hospitali ya wilaya ya Monduli, majengo ambayo yanakwenda kukamilisha hadhi ya hospitali ya wilaya na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma za afya ndani ya eneo lao.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.