Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Paul Christian Makonda, amewataka watumishi wa Kituo cha Huduma ya Pamoja Namanga kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya, kutumia technolojia za kisasa katika utendaji kazi ili kuharakisha utoaji wa huduma kwa wasafiri.
Mhe. Makonda amesema hayo alipotembelea Kituoni hapo na kutoridhishwa na utoaji wa huduma katika kituo ambacho ni muhimu kwa maingiliano na huduma ya usafiri na usafirishaji kati ya mataifa mawili ya Tanzania na Kenya yenye kuhusiana kibiashara na kijamii kwa muda mrefu hivi sasa.
Aidha, amebainisha kuwa huduma katika kituo hicho zinacheleweshwa na kuchukua muda mrefu kutokana na kutotumia teknolojia kikamilifu hasa katika ukaguzi wa Wageni na uidhinishaji wa mizigo, unaofanywa na taasisi za Serikali zilizopo kituoni hapo.
"Kituo cha Namanga kinatakiwa kuwa Kituo namba moja kati ya vituo vyte vya mipakani katika utoaji wa huduma bora kwa wageni na wasafiri, Ili kuongeza wigo wa mizigo na wageni wengi zaidi kuingia mkoani Arusha na hivyo kuchochea uchumi wa Arusha na Tanzania kwa ujumla wake" . Ameweka wazi Mhe Makonda
Ameongeza kuwa, suala ni muhimu katika kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya ukuzaji wa Utalii katika mkoa wa Arusha, ambapo anahimiza utoaji na upatikanaji wa huduma bora na rafiki kwa wateja Katika suala la matumizi ya teknolojia.
Ameutaka Uongozi wa Kituo cha pamoja Namanga kuwaunganisha wateja wao na mitandao ya simu ili wanapoingia nchini wawe na uwezo wa kuanza kutumia laini za simu kwa mitandao ya simu iliyopo nchini kwa kusajiliwa kupitia nyaraka wanazoziwasilisha kituoni hapo.
Awali, amewahimiza watumishi wa kituo hicho, kuwa mabalozi wazuri wa Utalii kwa kutoa huduma bora kwa wageni kwa kuwaeleza mazuri ya Tanzania pamoja na vivutio vya utalii vinavyopatikana Arusha ili kushiriki kikamilifu katika kuukuza Utalii na uchumi wa Tanzania.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.