Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amewataka watendaji mbalimbali wa serikali kuyaelewa vyema maono na ndoto za Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzitekeleza kikamilifu kwa wafanyabiashara na wawekezaji ili kuhakikisha kuwa taasisi za serikali haziwi sababu ya usumbufu na vikwazo kwa Wananchi.
Mhe. Paul Christian Makonda ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 04, 2024 wakati akizungumza na wawekezaji na watumishi wa kituo cha uwekezaji nchini Tanzania TIC wakati wa uzinduzi wa Kituo cha TIC kanda ya Kaskazini, kituo kilichozinduliwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo.
"Tusiwahudumie wawekezaji kama maadui, tuwe wawezeshaji. Itafika hatua tutaomba muongozo serikalini kwamba kabla hujateuliwa tukuulize ikiwa umewahi kufanya biashara yoyote ili iwe moja ya sifa kwasababu kuna watu hata biashara ya Kuku hawajawahi kuiweza lakini akiingia kwenye biashara za watu anasumbua utafikiri amekutana na shetani, anamshughulikia ili ampeleke motoni." Amesema Mhe. Makonda
Katika hatua nyingine Mhe. Paul Christian Makonda amesema ni matarajio yake kuwa kituo hicho cha uwekezaji Jijini Arusha kitakuwa kituo cha mfano barani Afrika kwa kuwa na huduma nzuri, za uhakika na za haraka ili kusaidia kuchochea uchumi wa Arusha na ukanda mzima wa Kaskazini mwa Tanzania.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.