Na Elinipa Lupembe.
Mgogoro wa muda mrefu wa mpaka baina ya Kijiji cha Buger na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, uliodumu zaidi ya miaka 15, hatimaye umetatuliwa na ufumbuzi wake kutangazwa rasmi na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K.Mongella.
Mhe. Mongella ametangaza utatuzi wa mgogoro huo, mara baada ya kazi aliyoiagiza kamati ndogo iliyoundwa ikijumuisha watalamu na wawakilishi wa kijiji cha Bugeli, kukamilika na kupata suluhisho la kudumu, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Buger.
Mhe. Mongella amesema kuwa, kamati imekuja na maamuzi ambayo yanagusa pande zote mbili, ambapo kila upande umeathirika kwa kumegwa eneo, huku eneo la hifadhi za Eka 8.3, wakiwachiwa wananchi pamoja na eneo lililojengwa nyumba tatu za wananchi, likiachiwa wananchi hao kuendelee kumiliki.
Amewasisitiza wananchi hao sasa kuachana na mgogoro na kujikita kufanya kazi za uzalishaji mali, shughuli ambazo zitaleta maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla wake na kuweka wazi kuwa eneo la kijiji na eneo la hifadhi yote ni mali ya Umma na kila mwananchi anayodhamana ya kuilinda ardhi hiyo.
"Kila mwananchi anawajibu wa kulinda eneo la hifadhi kwa kutambua thamani yake, ambayo wananchi wa Bugali wananufaika nayo, mnapata unyevuunyevu ambao unawawezesha kufanya kilimo cha mwaka mzima, hii ni kutokana na uwepo wa eneo la uhifadhi linalotunzwa, hivyo ni wajibu wetu kuendelea kutunza eneo hili kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo" Ameweka wazi Mhe. Mongella.
Aidha, ameuagiza uongozi wa Hifadhi hiyo, kuanza kuweka alama za mipaka 'bicon', kwa kuzingatia vipimo vya mipaka iliyokubalika na baada ya alama hizo kuweka barabata za kupitika ili wananchi watambue mipaka yao, ambayo itakuwa wazi kwa kila mtu.
Akisoma maamuzi ya Kamati, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi - ACC Eva Mallya, amesema kuwa mpaka huo umezingatia pande zote mbili ambapo takribani Eka 8.3 za hifadhi ambapo nyumba tatu za wananchi pamoja ja kisima cha maji zilizongia eneo la hifadhi limeachiwa wananchi huku baadhi ya vipande vya ardhi, ambavyo walikuwa wakilimwa vikirudi eneo la Hifadhi.
Naye Afisa Ardhi mkoa wa Arusha, Daniel Mruma, ameweka wazi kuwa, Idara ya ardhi imeshirikiana na timu iliyoundwa na Mkuu wa mkoa wa Arusha na pande zote mbili kufikia muafaka wa eneo la hifadhi kuachia Eka 8.3 na kazi inayofuata ni kuweka alama mpya za mipaka kwenye maeneo hayo.
Awali, mwezi uliopita Mkuu wa mkoa wa Arusha, alikutana na wananchi wa Buger na kujadili mgogoro huo na kuunda kamati ya makubaliano ambayo imekuja na maamuzi ambayo ndio suluhisho la kudumu la mgogoro huo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.