Na Daniel Gitaro
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya shule ya Sekondari Florian iliyopo Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.
Mradi huo unatekelezwa kwa fedha Kutoka Serikali Kuu, kwa ufadhili wa kampuni ya Barrick Gold Tanzania, ujenzi unaogharimu ya shilingi Milioni 458.1, ukijumuisha ujenzi wa vyumba 7 vya madarasa, mabweni mawili na matundu 11 ya vyoo.
Mhe. Mongella amewataka wasimamizi wa mradi huo pamoja na mafundi kuhakikisha, mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika kutokana na maelekezo ya Serikali.
"Simamieni mradi huu, ukamilike kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora, unaoendana na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali, ongezeni kasi ya usimamizi, ifikapo Janurai 2024 wanafunzi waanze masomo shuleni hapa". Amesisitiza Mhe. Mongella.
Akizungumza wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Mkuu huyo wa Mkoa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karatu, Juma Hokororo, ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kutekeleza na kuboresha miradi mbalimbali nchini.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali wananchi wake, na kuwaletea miradi mbalimbali hususani Sekta ya Elimu lakini pia shukrani za dhati ziwaendee wananchi wote walioshiriki kufanya kazi za ujenzi wa mradi huu”. Amesema.
Aidha, mradi huo ukikamilika utasaidia kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa pamoja na msongamano wa wanafunzi darasani uliokuwepo na kuwezesha wanafunzi wote kukaa katika mazingira rafiki na kusoma kwa utulivu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.