Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa huo, kubuni vyanzo endelevu vya mapato ili kuimarisha upatikanaji wa fedha za kuziwesha halmashauri hizo kujiendesha bila mikwamo.
Mhe. Mongella amewahimiza viongozi hao kuachana na vyanzo ambavyo havidumu na kufikiria namna ya kuwa na vyanzo ambavyo ni endelevu, vitaziwezesha halmashauri kujitegemea katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuwahudumia wananchi.
"Mnapaswa kuacha kutegemea vyanzo vya kuuza viwanja, ambavyo hupandisha makusanyo na pindi vinapokwisha mapato yanashuka, ushuru wa mazao sio vyanzo vya kuvitegemea havina uhakika pia, vinategemea mvua, hali ya hewa ikibadilika mapato yanayumba, jipangeni kutafuta vyanzo endelevu na sio hivyo vya kupita" Amesisitiza Mhe. Mongella.
Aidha amewatahadharisha wakurugenzi kuhakikisha usimamizi thabiti wa fedha za miradi inayoletwa kutoka serikali kuu, kwa kuzingatia maelekezo yake na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa fedha zilizoletwa na sio kuongeza fedha kutoka mapato ya ndani.
"Serikali inaleta fedha za miradi zikiwa na maelekezo kamili ya kukamilisha miradi, miradi kama ya TASAF, SEQUIP, P4R haiwezekani wengine wakamilishe na wengine waseme fedha hazitoshi, kila mkurugenzi ahakikishe anazingatia maeleekezo ya fedha za serikali na si vinginevyo" Amesisitiza Mhe. Mongella
Amekea tabia ya baadhi ya halmashauri kuchelewa kukamilisha miradi kwa kuwa serikali inatoa fedha za miradi zikiwa kamili na maelekezo ya utekelezaji, hivyo ni vema kila mkurugenzi na watalamu wakazingatia maelekezo ya utekezaji wa miradi inayoletewa fedha kutoka serikali kuu.
Naye Katibu Tawala Msaidizi Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi, Ramadhan Shaban Madeleka, amesema kuwa kikao kazi hicho chenye lengo la kujadili na kupitia utekelezaji wa Hoja za Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na kujadili masuala ya mapato na matumizi, usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya halmashauri.
Awali kikao kazi hicho kimewakutanisha Watalamu wa Idara za Fedha, Biashara, Maafisa Mipango, Ukaguzi wa Ndani kutoka halmashauri saba za mkoa wa Arusha, kimefanyika kwenye ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa mkoa Arusha.
#arushafursalukuki
#KaziInaendelea
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.