Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amewataka viongozi wa Wilaya ya Arusha na Halmashauri ya Jiji la Arusha kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili ikamilike kwa wakati.
Mhe. Mongella ameyasema hayo alipokuwa akikagua miradi ya elimu iliyochini ya mradi wa kuboresha na kuimarisha elimu ya awali na msingi (boost) katika jiji la Arusha.
Amesema, miradi ni mizuri ila kasi ya ujenzi ni ndogo hivyo wajitaidi kuongeza kasi ya ujenzi ili wakamilisha ujenzi wa miradi kwa wakati.
"Nataka muongeze kasi ya ujenzi na ifikapo Julai 20,2023 mnikabidhi miradi yote ikiwa imekamilika",alisema.
Amesisitiza kuwa serikali inaleta fedha nyingi za miradi hivyo niwajibu wa kila mmoja kuhakikisha fedha hizo zinatumika kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa amesema watayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa hasa lakusimamia miradi ya elimu ikamilike na kukabidhi ifikapo Julai 20,2023.
Nae, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Juma Hamsini amesema ataenda kuimarisha kitengo cha ujenzi ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati uliopangwa.
Ziara ya RC Mongella ilikuwa yakukagua miradi ya kuboresha miundombinu ya kidato cha sita katika shule ya Korona na mradi wa Boost katika shule ya Msingi Terrat na Msasani B ambapo kwa Mkoa mzima wa Arusha fedha kiasi cha bilioni 6.8 kilitolewa kwa ajili ya mradi wa Boost.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.