Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christia Makonda Paul Makonda amewataka Maafisa wa Taasisi za Ulinzi na watumishi wengine wa Umma Mkoani humo, kuwekeza kwenye fursa mbalimbali zinazopatikana mkoani hapa ikiwa ni maandalizi ya maisha baada ya kustaafu utumishi wa Umma.
Mhe. Makonda amesema hayo kwenye kikao kazi kilichowakutanisha Wakuu wa Taasisi za Ulinzi, kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa mkoa hup mapema leo Julai 11, 2024 na kuwataka Maafisa hao kutembelea ofisi za Kituo cha uwekezaji (TIC) iliyozinduliwa Mkoani Arusha, ili kujifunza na kuzielewa fursa zinazopatikana mkoani hapa na kuzitumia wakati wa utumishi wao, kabla ya kustaafu.
"Haitakuwa na heshima unakutana na mtu amestaafu halafu anaomba achangiwe hela ya matibabu, yaani unajisika vibaya kwamba hata uwezo wa kuwa na bima ya afya imekuwa changamoto, tumia akili ulizonazo za kuongoza taasisi kwenye kwenye familia yako, utalamu wako uakisi maisha yako" Amesema Mhe. Makonda.
Mhe. Makonda ameweka wazi kuwa, watumishi wa Umma wanapaswa kujiandaa na maisha ya kustaafu jambo ambalo linasaidia kuondoa migogoro, lawama na malalamiko ndani ya familia, kwa kufanya maandalizi familia zitaendelea kupata mahitaji muhimu hata baada ya kustaafu kwenye utumishi wa Umma.
Aidha, amesisitiza pia umaskini na shida zinasababisha kuongezeka kwa vitendo vya rushwa, uhalifu na uminywaji wa haki kwa baadhi ya watumishi wa umma, na hivyo kusisitiza dhamira ya kuwa na chanzo zaidi ya kimoja cha kuwaingizia kipato watumishi wa umma.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.