Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amethibitisha kuwa kwa idadi ya magari ya watanzania pekee waliojiandikisha kushiriki tukio la Land Rover Festival 2024, tayari rekodi iliyokuwa imeweka na Ujerumani mwaka 2018 kwa kuwa na magari chapa ya Land Rover 632 kwa wakati mmoja imevunjwa na kilichobaki ni kuthibitishwa na Kitabu cha rekodi duniani cha Guiness.
Mhe. Makonda ameyazungumza hayo mapema leo Oktoba 11, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Land Rover Festival 2024 inayotarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia kesho Jumamosi ya Oktoba 12, 2024 hadi Oktoba 14, 2024.
Mkuu wa Mkoa ambaye ni muasisi na muandaaji wa Tamasha hilo amewaambia wanahabari kuwa wanawania rekodi nyingine ya Guiness ya kuwa na magari mengi zaidi kwa wakati mmoja ndani ya hifadhi ya wanyamapori pamoja na rekodi ya kupaki magari ya Chapa moja kwa wakati mmoja ndani ya viwanja vya Magereza Kisongo Jijini Arusha.
Kaulimbiu ya tamasha hilo lenye nia ya kushirikisha magari zaidi ya 1000 kutoka ndani na nje ya Tanzania inasema "Shiriki uchaguzi wa serikali za Mitaa kwa maendeleo ya Taifa lako" ikihamasisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 kote nchini Tanzania.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.