Mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Arusha imetekeleza maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango wakuhakikisha wanapelekea mtambo wa kuchimba visima katika kijiji cha Sale.
Maelekezo hayo yalitolewa Mnamo Mei 18,2023 wakati Makamu wa Rais alipofanya ziara ya kikazi Wilayani Ngorongoro na kukutana na changamoto ya Maji katika Tarafa ya Sale.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya mtambo huo wa kuchimba visima Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Raymond Mwangwala ameishukuru RUWASA kwa kutekeleza maelekezo hayo kwa wakati.
Amesema kuletwa kwa Mtambo huo wa kuchimba Visima katika Tarafa ya Sale ni matokeo ya ziara hiyo ambayo italeta matokea makubwa ikiwemo kuondoa changamoto ya Maji.
Mwangwala amesema mtambo huo utachimba visima vyote katika Wilaya hiyo hasa yale maeneo ambayo yameshafanyiwa utafiti wa upatikanaji wa Maji.
Aidha, amewataka wanaojishughulisha na uchimbaji mabwawa pia nao wangeanza kazi yakuchimba kwani hata mifugo inahitaji maji.
Nae, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngorongoro Dkt. Juma Muhina,ameomba mtambo huo ukachimbe visima katika maeneo yote ya Wilaya hiyo na sio katika kijiji cha Sale pekeyake.
Amesema mtambo huo ni Mkombozi katika Wilaya hiyo kwani tatizo la maji ni kubwa hasa kipindi cha ukame na utawezesha upatikanaji wa Maji kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Arusha Joseph Makaidi amesema kwa kupatiwa mtambo huo kumerahisha hata kutekeleza maagizo hayo ya Mhe. Dkt. Philip Mpango kwani tayari walikuwa wameshapatiwa mtambo huo.
Mpango uliopo kupitia ilani ya CCM ni kuhakikisha vijiji vipate Maji kwa 85% au zaidi ifikapo 2025.
Amesema tatizo lililopo katika Kijiji cha Sale ni upungufu wa Maji hivyo mtambo huo unaenda kuongeza kiwango cha Maji kwa uchimbaji wa Visima vya kutosha.
Makaidi amesema Mtambo huo ni moja ya Mitambo 25 iliyotolewa na Serikali ya awamu ya sita ili viweze kufanya kazi ya kuleta Maji kwa wananchi kwa lengo la kumtua Mama ndoo kichwani.
RUWASA walipatiwa maelekezo ya ndani ya siku 3 kuhakikisha Mtambo huo ufike katika Kijiji cha Sale kwa ajili yakuanza kuchimba Visima na wameweza kutekeleza agiza hilo ndani ya muda.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.