Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella, akisalimiana na Katibu wa Tawi la CHADEMA, Israel Qima, Kijiji cha Gongali Kata ya Qutus, wakati alipotembelea mradi wa kitovu cha Teknolojia za Kihandisi (KITEKI), Wilaya ya Karatu leo tarehe 01 Desemba, 2023.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mongella alitoa fursa kwa wananchi wa kijiji hicho kutoa kero zao, ambazo waliainisha miongoni mwa kero kubwa ni ubovu wa barabara kutoka njia ya Mbulu - Tanki la kwa Basoro mpaka mwisho wa kijiji cha Gongali pamoja na mgogoro wa zahanati.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Gongali, Mhe. Joseph Baha, ameishukuru serikali kwa kujenga kituo hicho cha zana za kilimo, kituo ambacho licha ya kurahisisha upatikanaji wa zana hizo za kilimo, kitaongeza hamasa kwa wakulima na wafugaji na kungeza kasi ya uzalishaji wa mazao ya chakula na malighafi.
Mwenyekiti Baha, amesema kuwa licha ya mafanikio makubwa ya Serikali ya awamu ya sita, bado kijiji chao kinakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara inayoingia kwenye kijiji chao na mgogoro wa Zahanati ya kijiji kuwa katika Ofisi za Chama cha Mapinduzi.
Aidha, Mhe. Mongella ameuagiza uongozi wa TARURA kutengeza barabara hiyo na kukamilika kabla ya tarehe 31 Desemba, 2023, pamoja na kuahidi kushughulikia mgogoro wa zahanati ya kijiji iliyojengwa kwenye ofisi ya CCM.
Naye, Mwenyekiti wa CHADEMA tawi la Gongali, Israel Quima, ameipongeza Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa za kuleta maendeleo katika kijiji cha Gongali na amemuhakikishia Mhe. Mongella kuwa kwa sasa watanzania wanahitaji maendeleo na sio malumbano yanayotokana na itikadi za kisiasa.
"Mimi kama, Kiongozi wa CHADEMA, hatupingi maendeleo, maendeleo hayana chama, kama hakuna maendeleo tunapinga, na kama maendeleo yanakuja kijijini kwetu, hatuhitaji kuipinga serikali" Amesisitiza Quima
PICHA ZA MKUTANO
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.