Na Elinipa Lupembe.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Arusha, Mhe. Zaituni Swai amesema kuwa, Takwimu za matokeo ya Sensa ya watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022, yatawawezesha viongozi na waatalam wa mkoa huo, kupanga mipango thabiti ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 iliyozinduliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mhe. Zaituni ameyasema hayo, kwenye mkutano wa Mafunzo ya Usambazaji na Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 kwa viongozi wa makundi mbalimbali ya kijamii, mkoa wa Arusha, yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa AIM MALL Jijini Arusha leo tarehe 11 Desemba, 2023.
Amesema kuwa, matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 yalikuwa ni ya Kisayansi zaidi licha ya kuonesha idadi ya watanzania ni milioni 61 huku Idadi ya watu katika mkoa wa Arusha wamefikia 2, 356, 255, ameongeza kuwa takwimu hizo zimeenda mbali zaidi zikionyesha idadi na hali ya udumavu, idadi ya vituo vya kutolea huduma za kijamii, pamoja na idaidi ya vyoo bora.
Kupitia matokeo hayo, viongozi na waatalam wa mkoa wa Arusha kupanga mipango, itakayokwenda kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, ambayo imezinduliwa na Mhe. Rais wetu.
Aidha amewataka viongozi na wataalam waliohudhuria mafunzo hayo, kusikiliza kwa makini ili kuwa na uelewa wa pamoja juu ya usambazaji na matumzi ya Takwimu hizo muhimu kwa ngazi zote kuanzia mtu mmoja mmoja, wilaya, mkoa na hadi Taifa.
Mkutano huo umefunguliwa na Katibu Tawala Msaidizi Utumishi na Rasilimali Watu, mkoa wa Arusha, David Lyamongi kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Arusha, ukiwa na lengo la kuyajengea uwezo makundi mbalimbali ya kijamii juu ya matumizi sahihi ya matokeo ya Sensa ya watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022.
Makundi hayo ni pamoja na watalamu wa Mkoa na Serikali za Mamlaka ya Serikali za Mitaa, viongozi wawakilishi wa wananchi, viongozi wa Siasa, dini na mila, Watendaji wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, watendaji wa kata, kamati ya Sensa Mkoa pamoja na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo watu wenye mahitaji maalum.
#arushafursalukuki
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.