Na Jonas Kamaleki - Dodoma
Tanzania inajitosheleza kwa chakula kwa zaidi ya asilimia 120 na hivyo kuwa na uwezo wa kuuza chakula nje ya nchi.
Hii imetokana na Serikali kuwa na mipango madhubuti na kutekeleza mikakati ya kilimo cha kisasa hasa matumizi ya mbolea.
Hayo yamebainishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma leo tarehe 8/8/2024 katika kilele cha Siku ya Wakulima Nanenane.
Kilimo hapa Tanzania kinaendelea kupewa kipaumbele kwa kutengewa bajeti kubwa ambayo itatekeleza miradi mbalimbali ya umwagiliaji. Bajeti ya kilimo imetoka kwenye shilingi bilioni 294 hadi trilioni 1.248.
“Nawashukuru sana wakulima kwa kazi kubwa mnazozifanya za kulilisha Taifa”, alisema Rais Dkt. Samia.
Aidha, Dkt. Samia amesema kuwa bajeti ya mifugo imeongezwa kutoka shilingi bikini 60 hadi. zaidi ya bilioni 200.
Rais Samia amegawa matrekta 600 kwa wakulima na kuzindua kiwanda cha kuunganisha matrekta. Hii itapunguza gharama za kununua matrekta hayo.
Aidha, Rais Samia amesema ifikapo mwaka 2030 Serikali itakuwa imepeleka matrekta elfu 10 na power tiller elfu 10 kwa wakulima.
Katika kuhakikisha mazao yanahifadhiwa vizuri, Serikali imejenga maghala makubwa na ya kisasa katika mikoa mbalimbali nchini.
Maonesho ya Nanenane mwaka huu yamefanyika Kitaifa Dodoma baada ya kuzinduliwa tarehe 1/8/2024 na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufungwa leo tarehe 8/8/ 2024 na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mwisho.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.