Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 kwa Mkoa wa Arusha na ameaidi Serikali itahakikisha ilani ya CCM inakamilika.
Mawasilisho hayo ameyafanya kwa Halmashauri kuu ya chama Mkoa wa Arusha, katika ukumbi wa mikutano wa CCM Mkoa.
Amesema kila baada ya miezi mitatu Serikali itatoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya ambayo imo ndani ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Aidha, amekiomba Chama hicho kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mkoa katika kuleta maendeleo kwa wananchi hususani katika nyanja ya kukuza mapato ya Halmashauri kwa kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato.
Pia katika mpango wa kuwezesha kaya masikini (TASAF) amekiomba Chama kushirikiana na Serikali ili kuwabaini wanufaika husika wa mradi huo na kuwahamasisha wale waliokwisha kunufaika watoke wapishe wengine.
Akisisitiza zaidi Mhe. Mongella ameiyakikishia kamati hiyo ya Halmashauri kuu kuwa, kabla ya ukaguzi ujao miradi yote hususani ile ambayo serikali imetoa fedha zake inakamilika na kuanza kazi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha Mhe. Zelothe Steven ameitaka Serikali kuhakikisha kuwa kila sehemu ambayo miradi inatekelezwa wahakikishe wananchi wanapewa taarifa za kina kuhusu miradi hiyo ili wajue jinsi itakavyowanufaisha.
Pia, amesema Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha hakitakubaliana na mtu yoyote atakaefanya ubadhilifu wa aina yoyote kwenye miradi hiyo na watamchukulia hatua stahiki.
Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi imepokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM kutoka Serikalini ikiwa ni moja ya utaratibu uliowekwa katika ilani ya chama hicho wa kuikagua Serikali.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.