" Takwimu za Sensa ziende kubadilisha mfumo mzima wa nchi hasa kwa vijana kuangalia fursa zilizopo katika maeneo yao na kutengeneza ajira".
Kauli hiyo imetolewa na Kamisaa Mkuu wa Sensa Kitaifa Anna Makinda alipokuwa akizungumza na kamati ya sensa Mkoa katika kikao cha tathimini ya zoezi la sensa Mkoani hapo.
Amesema takwimu hizi ni muhimu sana katika kuisaidia Jamii kubadili utaratibu mzima wa maisha.
Ndio maana sensa ya mwaka huu ilijumuisha sensa ya watu na majengo ili kuonesha hali halisi ya maisha yetu watanzania.
Zoezi hili limefanikiwa kwa kiasi kikubwa Kitaifa hivyo tutegemee kuona Jamii nayo itatumia takwimu hizi katika kuleta maendeleo mbalimbali.
Kufanikiwa kwa zoezi hili la sensa kumetokana na utendaji wa kizalendo na umoja baina yetu.
Takwimu za sensa zikasaidie kuondoka migogoro ya mipaka na migogoro mingine mingi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amesema kwa Mkoa wa Arusha zoezi lilienda vizuri na kwa mafanikio makubwa.
Aidha, ameishauri Ofisi ya Taifa Takwimu kuendelea kutoa elimu juu ya sensa ili kujenga uwelewa zaidi hasa ngazi za chini na kurahisisha zoezi lijalo kwani Jamii itakuwa na uwelewa wa kutosha.
Amesema takwimu za sensa zitasaidia kuleta maendeleo katika Jamii.
Nae,Mratibu wa sensa Mkoa wa Arusha Leocardia Mtei amesema zoezi la sensa limefanyika vizuri na kwa ushirikiano mkubwa sana.
Kikao cha tathimini ya sensa kimefanyika Mkoani Arusha na Kamisaa wa sensa akiwashukuru wote kwa ushirikiano waliouwonesha hadi zoezi kukamilika vizuri.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.