OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema serikali haitavumilia ukiukwaji sheria na hatua kali zitachukuliwa kwa watumishi watakaobainika kukiuka sheria kwenye ukusanyaji mapato ya serikali.
Mhe.Mchengerwa ameyasema hayo bungeni leo alipokuwa akitoa ufafanuzi wa malalamiko yaliyotolewa bungeni wiki iliyopita na Mbunge wa Msalala (CCM), Idd Kassim kuwa Mamlaka za Seikali za Mitaa zinatoza ushuru mashambani na wafanyabishara wasiolipa wanapewa adhabu kali na kupigwa.
Akitoa ufafanuzi, Waziri Mchengerwa ameliambia bunge kuwa ushuru wa mazao hutozwa kwa Mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290 na vifungu vya 6,7,8 na 9 vya sheria hiyo ushuru wa mazao ni moja ya vyanzo vya mapato kwa mamlaka za miji, halmashauri za wilaya, mamlaka za miji midogo na halmashauri za vijiji.
Aidha, amesema kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa,Sura ya 290 ushuru huo unatozwa kwa asilimia tatu ya bei ya kununulia shambani kwa mazao ya chakula na biashara.
“Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290, inatamka kuwa ushuru huu unalipwa na mnunuzi wa zao alilonunua kutoka kwa mkulima kwa kiwango cha asilimia tatu ya bei ya kununulia shambani, endapo mfanyabiashara atanunua mazao hayo kutoka shambani kwa mkulima, atapaswa kulipa ushuru huo katika eneo hilo ambalo ununuzi umefanyika,”amesema.
Kadhalika, amesema ununuzi ukifanyika sokoni ushuru utatozwa katika soko hilo. Aidha, mazao yanapotoka nje ya Halmashauri yanapaswa kuwa yamelipiwa ushuru na endapo itabainika mfanyabiashara anayetoa mazao nje ya Halmashauri pasipo kuwa na risti halali ya malipo ya ushuru, atapaswa kulipa ushuru wa mazao husika na faini.
“Aidha Mkulima anayesafirisha mazao chini ya tani moja amesamehewa kulipa ushuru huo. Ninaomba kutoa rai kwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia sheria hiyo kwa kuzingatia maslahi mapana ya pande zote mbili, yaani upande wa mnunuzi na upande wa mnunuzi na upande wa Halmashauri’ amesema
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.