Na Elinipa Lupembe
Vijana 23 wa Skauti waliojitolea kutembea na kuhamasisha utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji nchini, kwa kufanya matembezi ya hiari kuelekea kilele cha wiki ya vijana na kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 mkoani Manyara, wametakiwa kuhamasisha jamii bila kuchoka suala zima la utunzaji wa mazingira.
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Arusha, Mhe. Felician Mtahengerwa, kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Arusha wakati wa kuwapokea vijana hao 23 wa skauti wakitokea mkoa wa kilimanjaro kupanda mlima Kilinjaro wakielekea mkoani Manyara kwenye kilele cha mbio za Mwenye wa Uhuru 2023.
Mhe. Mtahengerwa, licha ya kuwapongeza vijana hao kwa uzalendo wa kujitoa kuhamasisha jamii katika utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji, amewata kuhamasisha jamii husuani vijana wenzao kuhakikisha wanajikita katika utunzaji wa mazingira kwa kuwa ndio rasilimali kuu kwa binadamu na viumbe wote.
"Niwapongeze kwa uzalendo mlioonesha lakini pia mnapaswa kutambua vijana mnalo jukumu kubwa la kulitumikia Taifa kwa kuhamasisha jamii umuhimu na faida za utunzaji wa mazingira, kwa kutambua kuwa mazingira ni uhai wa viumbe vyote ikiwemo wanadamu" Amesema Mhe. Mtahengera
Hata hivyo vijana hao wameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa vijana fursa na vipaumbele vingi kushiriki katika ujenzi wa taifa pamoja na kushiriki kwenye shughuli mbalimblai za kijamii na za maendeleo nchini.
Mratibu Mkuu wa Zoezi la Kizalendo, Kamishna wa Skaut wilaya ya Bariadi, Mayunga Kidoyayi amesema kuwa lengo la matembezi hayo ya hiari ni kuendelea kuikumbusha jamii jumbe za Mwenge wa Uhuru 2023 uliobeba kauli mbiu Tunza Mazingira, okoa vyanzo vya maji kwa Ustawi wa viumbe hai kwa uchumi wa Taifa.
Amesema kuwa Mwenge wa Uhuru 2023 umepita mikoa yote ya Tanzania ukiwa na jumbe mbalimbali lakini vijana hao wanapita kuikumbusha na kuhamasiha jamii kuzingatia jumbe hizo ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa, kujinga na magonjwa ya UKIMWI na Malaria, umuhimu wa lishe bora, kupiga vita matumizi ya Madawa ya Kulevya pamoja na utunzaji wa mazingira kwa maendelo ya jamii na uchumi wa Taifa.
Kiongozi wa Kikosi Maalum cha Skaut, Omary Ahmed Kasaka, amesema kuwa wao kama vijana wamepita kuelekea mlima Kilimanjaoro na kuielemisha jamii umuhimu wa kutunza mazingira hususani wananchi waishio pembezoni mwa mlima Kilimanjaro, ambao mara nyingi kunatokea moto unaosababishwa na shughuli za kibainadamu.
"Sisi kama vijana wa kitanzania, tunaridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na Mhe. Rais hivyo tuko tayari kujitoa kuunga mkono juhudi zote za serikali, tunakwenda Manyara kwa kutembea kwa mguu Km 162, kushiriki kilele cha wiki ya Vijana, kumbukumbu ya Mwl. Jk Nyerere pamoja na kiele cha Mbio za mwenge wa Uhuru 2023" Amesema Omary Ahmed Kasaka
#ARUSHA FURSA LUKUKI
#KaziInaendelea
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.