Watumishi wa Umma wametakiwa kuwa na kawaida ya kupima Afya zao, kufanya mazoezi, kuepuka misuguano isiyo ya lazima mahala pa kazi pamoja na migogoro ya kifamilia ambayo imeonekana ndiyo kiini kikubwa cha msongo wa mawazo ambapo hupelekea kushusha ufanisi wa utendaji kazi Serikalini.
Hayo yamesemwa na John Mongella,Mkuu wa Mkoa wa Arusha wakati akichangia mada ya Uongozi Binafsi na Akili Hisia katika Mafunzo kazi ya Viongozi wa Mkoa wa Arusha yanayoendelea katika Hotel ya The Retreat At Ngorongoro iliyopo Wilayani Karatu.
Mongella amesema ili kuwa Taasisi imara sharti watu wake wakawa na afya njema ya kiakili pamoja na utimamu wa kimwili kwani vitu hivyo ndiyo msingi wa utendaji kazi mzuri na kuwataka Watumishi kuepuka kujiingiza katika tabia zinazochangia msongo wa mawazo ikiwemo misuguano isiyo ya lazima mahala pa kazi, migogoro ya ndoa, tamaa ya kupata mali harakaraka na madaraka pamoja na ulevi uliyokithiri.
Aidha,katika mafunzo hayo Viongozi washiriki wamepata fursa ya kujifunza na kutafakari mambo mbalimbali ya kiuongozi ikiwemo namna ya kukabiliana na changamoto za msongo wa mawazo mahali pa kazi na katika familia,namna ya kutumia vizuri rasilimali watu ili kuleta matokea chanya ya kiutendaji na pia namna ya kufanya kazi umoja na mshikamano.
Mafunzo hayo ya siku nne yana lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji Viongozi wa Mkoa wa Arusha yamejumuisha Viongozi wa kada mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa,Katibu Tawala Mkoa,Wakuu wa Wilaya,Wakuu wa Seksheni na Vitengo toka Sekretariati ya Mkoa, Makatibu Tawala Wilaya,Meya wa Jiji la Arusha na Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri,Wakuu wa Taasisi za Umma Mkoa wa Arusha pamoja na Wakuu wa Seksheni na Vitengo toka Halmashauri ambapo mafunzo hayo yalifunguliwa jana tarehe 13/08/2023 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Anjella Kairuki.
Mada hizo za Uongozi Binafsi na Akili Hisia zimetolewa na Bi.Zuhuru Muro mkufunzi toka Uongozi Institute pamoja na Dkt.Garvin Kweka toka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.